Na Joseph Ngilisho-Arusha
ARUSHA: Kundi la tatu na la nne lenye jumla ya washtakiwa 101 wa uchaguzi, wakiwemo watu wenye ulemavu wa kuongea 'BUBU', mwandishi wa habari na wanaodaiwa kuwa wanafunzi, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa ajili ya kutajwa kwa kesi ya uhaini na kula njama za kuiangusha Serikali iliyopo madarakani.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Erasto Phill, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali alidai kuwa upelelezi wa kesi hizo bado haujakamilika, hivyo kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Utekelezaji wa kauli ya Rais waulizwa
Katika utetezi, jopo la mawakili likiongozwa na Wakili Hamis Mkindi, lilihoji kutotekelezwa kwa kauli ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kuachiwa huru kwa washtakiwa ambao hawahusiki na makosa hayo.
Aidha, Mkindi alihoji uwepo wa watoto na wanafunzi walio chini ya miaka 18 wanaodaiwa kushikiliwa mahabusu kinyume cha sheria, akisisitiza kuwa jambo hilo linapaswa kutazamwa kwa haraka ili kuepusha ukiukwaji wa haki za watoto.
TANGAZO:PATA OFFER KUTOKA KAMPUNI YA UTALII YA RIBRIS SAFARIS
Makundi ya awali yaendelea kuahirishwa
Kesi za makundi ya kwanza na ya pili zenye jumla ya washtakiwa 79, ambazo zilisikilizwa jana, pia ziliahirishwa hadi Desemba 3, 2025 kutokana na upelelezi kutokamilika.
Katika muendelezo wa mwenendo wa kesi za leo, Wakili wa Serikali Gilbart Msuya aliieleza mahakama kuwa hata katika makundi ya leo upelelezi bado haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Kesi mbili kuu zikiahirishwa
Kesi namba 26446/2025 yenye washtakiwa 53, wanaokabiliwa na mashitaka ya kula njama na vitendo vya uhaini, iliahirishwa hadi Desemba 3, 2025 kutokana na upelelezi kutokamilika.
Kundi la nne la washtakiwa 63 katika kesi hiyo hiyo (26446/2025) lilipandishwa kizimbani na kesi hiyo ikaahirishwa hadi Desemba 4, 2025.
Hakimu Erasto Phill aliuagiza upande wa Jamhuri kufanya uchambuzi wa kina ili kubaini kama kweli wapo watoto walio chini ya miaka 18 wanaoshikiliwa mahabusu kinyume cha sheria, na kuwasilisha taarifa hizo katika tarehe inayofuata ya kutajwa.
Makundi mengine bado yanakuja,
Taarifa kutoka ndani ya vyanzo vya kimahakama zinaeleza kuwa kundi la tano na la sita la washtakiwa wa kesi hizo za uhaini linatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo Jumatatu ijayo, kuendeleza mfululizo wa uwasilishaji wa makundi mbalimbali mbele ya mahakama
Nje ya mahakama, hali iligubikwa na simanzi baada ya jamaa na ndugu wa washtakiwa kuangua kilio walipoona wapendwa wao wakipakiwa kwenye magari ya magereza.
Baadhi yao walitoa ombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili kuangalia kwa huruma hatima ya ndugu zao, wakisema familia nyingi zimeathirika, watoto wakikosa msaada wa wazazi wao walioko mahabusu.
Ends.










0 Comments