Na Joseph Ngilisho, Arusha
Serikali, sekta binafsi na wananchi wametakiwa kushirikiana kikamilifu katika mapambano dhidi ya ubadhilifu, rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma, kwa kuwa jukumu hilo haliwezi kuachiwa upande mmoja pekee.
Kauli hiyo imetolewa na Ramadhani Madeleka, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, wakati akifunga Kongamano la Mwaka la Mapambano dhidi ya Rushwa na Ufisadi lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Madeleka alisema mapambano dhidi ya rushwa na udanganyifu yanahitaji nguvu ya pamoja, uadilifu wa watumishi wa umma, na ushiriki wa wananchi ili kujenga mifumo madhubuti itakayozuia mianya ya ufujaji wa fedha za serikali.
> “Tumeelezwa na tumejifunza kwamba mapambano dhidi ya udanganyifu si jukumu la mtu mmoja. Ni wajibu wa pamoja. Mawazo na mapendekezo tuliyoyapata yasibaki kwenye kabrasha—yanapaswa kuingizwa katika sera na taratibu za kila siku ili kuongeza uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi zetu,” alisema Madeleka.
Alisisitiza umuhimu wa wataalamu na watumishi waliotoka katika kongamano hilo kuhakikisha maarifa waliyopata yanatekelezwa kwa vitendo, hasa katika usimamizi wa fedha za umma, taratibu za manunuzi, na mifumo ya ugavi ili kuzuia vitendo vya udanganyifu.
Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Wataalamu wa Udhibiti wa Udanganyifu Tanzania (ACFE), Ally Mabrouk, alisema kongamano hilo la siku nne limekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mpya za kukabiliana na udanganyifu.
> “Kupitia ACFE tumejifunza kwamba kudhibiti udanganyifu si jukumu la taasisi za serikali pekee. Sekta binafsi nayo ina wajibu mkubwa, kwani ubadhilifu unapotokea huathiri pande zote. Juhudi hizi pia zinaunga mkono ajenda za serikali kuhusu utawala bora, uwazi na uwajibikaji,” alisema Mabrouk.
Kongamano hilo lililowakutanisha wataalamu wa udhibiti wa udanganyifu kutoka sekta mbalimbali—serikali, taasisi binafsi na mashirika ya kimataifa—lililenga kuimarisha ushirikiano na kutoa mbinu mpya za kupambana na changamoto zinazotokana na udanganyifu unaobadilika kwa kasi kutokana na teknolojia.
Kupitia mada mbalimbali, washiriki walipata fursa ya kutathmini mifumo ya ndani ya taasisi zao na namna ya kuiboresha ili kuongeza uwazi na kujenga mifumo ya uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma na binafsi.
-ends...










0 Comments