BODI MPYA YA TANAPA INVESTMENT LIMITED YAZINDULIWA: JENERALI WAITARA AITAKA KUIMARISHA UBUNIFU NA UWAZI KATIKA UWEKEZAJI

Na Joseph Ngilisho – Arusha


Bodi ya Wakurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA Investment Limited – TIL) imezinduliwa rasmi leo jijini Arusha na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa TANAPA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali George Marwa Waitara.


Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Jenerali Waitara aliipongeza bodi mpya kwa kuaminiwa kuongoza kampuni hiyo muhimu, huku akisisitiza umuhimu wa uongozi wa kitaalamu, uwajibikaji na uwazi katika kusimamia miradi yote ya uwekezaji wa kampuni hiyo.

> “Bodi ya Wadhamini inawapongeza kwa kuchaguliwa kuongoza kampuni hii. Twendeni pamoja kusimamia kwa weledi na uwazi miradi yote ya kampuni. Tukaimarishe ushirikiano kati ya kampuni, TANAPA na wadau kwa misingi ya uwajibikaji, ubunifu na uadilifu,”alisema Jenerali Waitara.


Aliongeza kuwa bodi hiyo mpya inatarajiwa kuwa nguzo ya mageuzi ya kiuwekezaji, ikileta ubunifu katika miradi yenye tija, kuimarisha taswira ya kampuni hiyo serikalini na katika sekta binafsi, na kuendesha miradi itakayochochea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 – hasa katika eneo la uhifadhi endelevu unaowanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.

TANAPA YASIFIA MABADILIKO YA UWEKEZAJI CHINI YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, CPA Mussa Nasoro Kuji, alisema Shirika linaendelea kunufaika na mazingira bora ya uwekezaji yanayowezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara wa mageuzi katika sekta za uhifadhi, utalii na uwekezaji wa miundombinu.

> “Serikali imeweka mazingira rafiki yanayovutia uwekezaji katika sekta ya uhifadhi. TANAPA Investment Limited itakuwa chombo muhimu katika utekelezaji wa miradi mikubwa yenye tija, inayolenga kuongeza mapato ya Shirika na kulinda maliasili zetu,”alisema CPA Kuji.


TIL YAJIPANGA KUONGOZA MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA KATIKA UWEKEZAJI

Naye Mtendaji Mkuu wa TANAPA Investment Limited, Mhandisi Dkt. Richard Matolo, alisema kampuni hiyo inajipanga kutumia teknolojia za kisasa na utaalamu wa hali ya juu ili kuboresha ubora na ufanisi wa miradi yote itakayoisimamia.

> “Tumejipanga kuleta mapinduzi katika sekta ya ukandarasi na uwekezaji. Tutatumia mbinu za kitaalamu na ubunifu ili kuongeza tija, kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati, kwa viwango vya juu na kwa gharama nafuu,”alisema Dkt. Matolo.


KUHUSU TANAPA INVESTMENT LIMITED (TIL)

TANAPA Investment Limited ni kampuni tanzu ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) iliyoanzishwa kwa lengo la kusimamia miradi ya uwekezaji wa kimkakati inayohusiana na uhifadhi, utalii na maendeleo ya miundombinu.
Kampuni hiyo inalenga kuongeza mapato yasiyo tegemezi moja kwa moja na bajeti ya Serikali, huku ikihakikisha miradi yote inatekelezwa kwa kuzingatia kanuni za uwajibikaji, uadilifu na uendelevu wa mazingira.

Uzinduzi wa bodi hiyo mpya unatarajiwa kuimarisha utendaji wa kampuni hiyo katika kutekeleza miradi ya kimkakati ndani na nje ya hifadhi, na hivyo kuongeza mchango wake katika maendeleo ya taifa.





– MWISHO –

Post a Comment

0 Comments