VIGOGO WANNE WA CHADEMA AKIWEMO HECHE WAACHIWA HURU,MARIDHIANO YA KISIASA YANUKIA

By Arushadigtal -Dar 


Jeshi la Polisi limewaachia kwa dhamana baadhi ya viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akiwemo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche.

Kwa mujibu wa wakili wao, Hekima Mwasipu, viongozi hao waliachiwa jioni ya leo, Jumatatu Novemba 10, 2025, na wanatakiwa kuripoti tena kesho Jumanne saa tano asubuhi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.

Mbali na Heche, waliyoachiwa ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, na Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob (Boni Yai).

Lema, Golugwa na Boni Yai ni miongoni mwa viongozi waliokamatwa hivi karibuni wakidaiwa kuhusika na maandamano yaliyopelekea vurugu kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, katika baadhi ya mikoa ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Songwe, Kilimanjaro, Dodoma, Mara na Ruvuma.

Heche alikamatwa tangu Oktoba 22, 2025, nje ya Mahakama Kuu Dar es Salaam, alipokuwa akielekea kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini.

Wakati huo Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, jioni hii kimethibitisha kuwa Viongozi wake waliokuwa wanawashikiliwa na Jeshi la Polisi ambao ni John Heche, Amani Golugwa, Godbless Lema na Boniface Jacob, wameachiwa kwa dhamana.


“Nilikuwa nawasimamia Viongozi wa CHADEMA ambao walikamatwa siku za hivi karibuni na kuhifadhiwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, wameambiwa wakaripoti kesho saa 5 asubuhi” —— Wakili wa CHADEMA, Hekima Mwasipu. 

Post a Comment

0 Comments