Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ametoa agizo kwa wamiliki wote wa gereji bubu jijini Arusha kujisalimisha mara moja ndani ya mwezi mmoja katika mamlaka husika ili kubainika usajili wao na kuunganishwa na wenzao wanaofanya kazi katika maeneo yaliyopangwa rasmi na serikali.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za mafundi wa gereji katika eneo la Suye, Kata ya Kimandolu, DC Mkude alisema serikali haitavumilia uendeshaji wa biashara holela zisizo na utambulisho wa kisheria, huku akiahidi kumaliza changamoto zinazowakabili mafundi hao, ikiwemo tishio la kunyang’anywa eneo lao na Halmashauri ya Jiji la Arusha.
> “Mimi si mtu wa maneno, bali vitendo. Nitahakikisha mnapata hati miliki ya umoja wenu na si kwa mtu mmoja mmoja, ili fani hii iwe endelevu na manufaa yake yawafikie kizazi hiki na kijacho,” alisema Mkude.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwawezesha mafundi hao kwa kuwapatia wataalamu watakaowasaidia katika mchakato wa kupata mikopo kupitia Halmashauri ya Jiji, ili wawe miongoni mwa wanufaika wa fedha za maendeleo zinazotolewa kwa vijana na wajasiriamali wadogo.
> “Nitahakikisha mnapatiwa mtaalamu wa kuwasaidia kupata mikopo, maana matamanio yangu ni kuona nanyi mnainua kipato chenu na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Mkude.
Hata hivyo, DC huyo alitoa onyo kali kwa waendesha bodaboda wanaoendelea kuendesha pikipiki zao zikiwa na viripuzi na milipuko ya injini, akisema tabia hiyo inaleta usumbufu na taharuki kwa wananchi.
> “Kuanzia sasa, yeyote atakayekamatwa akiendesha pikipiki yenye mlipuko atatozwa faini isiyopungua shilingi milioni moja (Sh1,000,000). Sheria ndogo itatungwa rasmi kuhakikisha nidhamu inarudi barabarani,” alisisitiza Mkude.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Mafundi wa Gereji Krokoni, Godfrey Majangu, akisoma risala yao mbele ya Mkuu wa Wilaya, alisema wanaamini ziara hiyo itakuwa mwarobaini wa changamoto zilizowakabili kwa muda mrefu.
Majangu alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa hati ya umiliki wa eneo, miundombinu mibovu, pamoja na ukosefu wa mikopo ya kuwawezesha mafundi kuendeleza shughuli zao.
> “Lengo letu kuu ni kuongeza idadi ya vijana wanaojifunza ufundi, ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Tunaamini tukipata ushirikiano wa serikali, tunaweza kuwa chachu ya maendeleo,” alisema Majangu.
Naye Mgombea Udiwani wa Kata ya Kimandolu, Abraham Mollel, aliiomba TARURA na TANROADS kushughulikia kwa haraka tatizo la makorongo na miundombinu mibovu katika eneo hilo, akisema hali hiyo imekuwa kikwazo kwa wananchi na wateja wanaofika kwenye gereji hizo.
> “Tunaiomba TARURA na TANROADS washughulikie haraka tatizo la makorongo na barabara hizi duni. Hii itarahisisha shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wetu,” alisema Mollel.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Wilaya ililenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wajasiriamali wadogo, pamoja na kusikiliza changamoto zinazokwamisha sekta ya ufundi magari katika jiji la Arusha, ambapo mafundi hao waliapa kuendelea kushirikiana na serikali katika kukuza uchumi wa eneo hilo.
Ends...








0 Comments