PIGO LINGINE KWA MAWAKILI WA SERIKALI KESI YA UHAINI YA TUNDU LISU

By Arushadigital -Dar 

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa uamuzi mdogo (ruling) kufuatia pingamizi lililowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, katika kesi yake ya uhaini inayoendelea Mahakamani hapo.


Pingamizi hilo lilihusu kupinga kuwasilishwa Mahakamani kwa taarifa ya uchunguzi wa picha jongefu (video) iliyotolewa na shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri, Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Samwel Elibariki Kaaya.


Kesi hiyo iliendelea leo Alhamisi, Oktoba 23, 2025, mbele ya jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Danstan Ndunguru.

Katika hoja zake, Lissu alieleza kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kutoa report bali certificate pekee, kwa mujibu wa taratibu za kisheria. Aidha, alidai kuwa shahidi huyo alipaswa kuandaa picha mnato (still pictures) za video husika, baada ya kuteuliwa rasmi na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) au Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kupitia tangazo la serikali.


Kwa upande wa Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema, alijibu vikali hoja hizo akieleza kuwa Mahakama haina wajibu wa kufungwa na uamuzi wake wa awali wa Oktoba 22, 2025, uliokataa kupokea Memory Card na Flash Disk kama vielelezo.

Mrema aliongeza kuwa mshtakiwa amekiuka maelekezo ya Mahakama kwa kusoma maudhui ya taarifa hizo za uchunguzi kabla ya kupokelewa rasmi Mahakamani, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa kisheria. Aliiomba Mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo.


Hata hivyo, katika kujibu hoja hizo, Lissu alisisitiza kuwa Mahakama tayari ilishakataa kupokea Memory Card na Flash Disk hizo, hivyo taarifa ya uchunguzi inayotokana na vielelezo hivyo haiwezi kuwa na uhalali kisheria.


Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Ndunguru alitangaza kuwa Mahakama imekubaliana na hoja za mshtakiwa, na hivyo kielelezo hicho kimekataliwa rasmi.

Kesi hiyo inaendelea.

#Arushadigital-Update#



Post a Comment

0 Comments