MAFUNDI GARAGE SUYE WAAHIDI KUTIKI KWA WINGI OKTOBA 29,WAKOSHWA NA DC MKUDE KUTATUA KERO ZAO AWAAHIDI KUWAMILISHA ENEO LA HALMASHAURI KUPITIA VIKUNDI VYAO.

 UMAKRO WAAPA KUJITOKEZA KUPIGA KURA, DC MKUDE AWAHIDI MIUNDOMBINU, UJENZI WA CHOO NA KIVUKO KIPYA

Na Joseph Ngilisho, Arusha



UMOJA wa Mafundi Magari wa Krokoni (UMAKRO) uliopo Suye, Kata ya Kimandolu jijini Arusha, umeahidi kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, wakieleza dhamira yao ya kuchagua viongozi watakaosimamia maendeleo, ustawi wa wananchi na ustahimilivu wa sekta ya ajira.

Ahadi hiyo imetolewa mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alipokutana na zaidi ya mafundi 300 wa umoja huo kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kutoa majibu ya serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayowakabili, ikiwemo miundombinu, usafi wa mazingira na hofu ya kuondoshwa katika eneo lao la kazi.


Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mwenyekiti wa UMAKRO, James Agustino, alisema kumekuwa na changamoto kubwa kati yao na Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhusu uhalali wa uwepo wao katika eneo la Suye, jambo lililosababisha hofu ya kuhamishwa kwa madai ya kutokuingiza mapato ya kutosha.

> “Tulihamishiwa hapa Suye mwaka 2006 kutoka Krokoni katikati ya jiji. Wakati tunawasili, hapakuwa na miundombinu yoyote. Tuliwekeza nguvu na fedha kuboresha eneo hili, tukajenga vibanda vya kujisitiri na mvua, tukazungusha ukuta kwa usalama wa mali zetu na magari ya wateja,” alisema Agustino.


Aliongeza kuwa kwa sasa kila fundi analipa Sh15,000 kwa kibanda cha biashara na Sh80,000 kwa kila “gate” ya gereji, makubaliano yaliyofikiwa na halmashauri ya jiji. Hata hivyo, alisema wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kukosa control number za malipo, jambo linalowatia hofu ya kuondoshwa katika eneo hilo.


Kupitia risala iliyosomwa na Katibu wao, Godfrey Majango, mafundi hao walisema wana mpango wa kupanua huduma zao kwa kuanzisha teknolojia za kisasa za matengenezo ya magari, kuongeza idadi ya vijana wanaopata mafunzo ya ufundi na kuanzisha kituo maalum cha mafunzo ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Aidha, walieleza kuwa barabara inayoingia katika eneo la gereji hiyo ni mbovu kiasi cha kuwa kero kubwa wakati wa mvua za masika, jambo linalowazuia wateja kufika kwa urahisi.

Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Wilaya Mkude aliwahakikishia mafundi hao kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami mara baada ya shughuli za uchaguzi kumalizika.

> “Serikali inatambua mchango wenu mkubwa katika kukuza ajira na pato la wananchi. Baada ya uchaguzi, tutajenga barabara hii kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli zenu,” alisema Mkude.


DC Mkude pia alieleza kuwa tayari serikali imefanikisha marekebisho ya kivuko cha maji kilichokuwa kikiwasumbua wananchi na wateja wanaoingia eneo la Suye, hatua iliyopunguza adha ya usafiri hasa wakati wa mvua.

Vilevile, aliahidi kujenga choo cha kisasa katika eneo hilo ili kuboresha usafi na afya ya mafundi pamoja na wateja wao.

Katika hatua nyingine, Mkude aligusia kero ya waendesha pikipiki (bodaboda) wanaoendesha huku wakipiga kelele za milipuko ya injini, hali inayosababisha taharuki kwa wananchi na kuvuruga utulivu wa jiji.



> “Natoa maelekezo kwa Baraza la Madiwani lijalo kutunga sheria ndogo maalum itakayotoa adhabu kali kwa watakaokamatwa wakiendesha pikipiki huku wakisababisha milipuko na kelele. Faini isiwe chini ya shilingi milioni moja (Sh1,000,000) kwa kila atakayebainika kufanya vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani,” alisisitiza DC Mkude.


Aidha, kuhusu ombi la umiliki wa eneo lao, DC huyo alisema ataliwasilisha katika Baraza jipya la Madiwani baada ya uchaguzi ili liweze kutoa uamuzi wa kuwamilikisha eneo hilo kupitia umoja wao wa UMAKRO badala ya mtu binafsi

"Mimi si mtu wa maneno, bali vitendo. Nitahakikisha mnapata hati miliki ya umoja wenu na si kwa mtu mmoja mmoja, ili fani hii iwe endelevu na manufaa yake yawafikie kizazi hiki na kijacho,” alisema Mkude.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na vijana hao katika kuwawezesha kupata mitaji kupitia taasisi za kifedha na mabenki, ili kukuza zaidi shughuli zao za kiuchumi.

> “Tutazungumza na taasisi za kifedha ili muweze kupata mikopo kwa masharti nafuu kupitia vikundi vyenu. Serikali ipo pamoja nanyi kuhakikisha kila kijana anakuwa sehemu ya maendeleo ya nchi,” alisema Mkude.


Ziara hiyo ililenga kuimarisha uhusiano kati ya serikali na wajasiriamali wadogo, huku mafundi hao wakiahidi kuendelea kushirikiana na serikali kujenga Arusha mpya yenye ajira endelevu, miundombinu bora na nidhamu ya kijamii.









Ends..

Post a Comment

0 Comments