TAHARUKI MAHAKAMANI KESI YA UHAINI YA LISU,MMOJA AJITOA FAHAMU NA KUDAI AMETUMWA NA MUNGU

 By Arushadigital -Dar 


Taharuki ilitokea leo katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, wakati wa kuanza kwa usikilizwaji wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, baada ya mtu mmoja aliyekuwapo ukumbini kuanza kupaza sauti akidai anataka kutoa “ujumbe wa maono” kwa majaji.


Tukio hilo lilitokea saa 3:24 asubuhi, wakati jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, likisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, likiingia kusikiliza kesi hiyo katika ukumbi wa wazi namba moja wa Mahakama hiyo.



Mara baada ya majaji kuingia, mtu mmoja aliyekuwa amekaa juu ya chumba hicho alianza kupaza sauti kwa nguvu akisema anataka kutoa ujumbe wa maono, hali iliyosababisha taharuki na kusimamisha shughuli za Mahakama kwa muda.


Jaji Ndunguru aliamuru askari waliokuwapo ndani ya ukumbi huo kumtoa nje mtu huyo ili vikao viendelee. Hata hivyo, alipoamrishwa kutoka nje, mtu huyo alianza kukemea kwa jina la Yesu, akiwazuia askari Magereza waliokuwa wakijaribu kumshika, hali iliyozidisha msisimko ukumbini huku baadhi ya watu wakisimama na kushuhudia tukio hilo.


Kutokana na hali hiyo, Jaji Karayemaha alilazimika kutoa onyo kwa watu waliokuwa ukumbini, akiwataka waache kupiga picha na kukaa chini, akisisitiza kuwa Mahakama inaendelea na shughuli zake.


Baada ya askari kufanikiwa kumtoa mtu huyo nje, hali ilirejea kuwa ya utulivu, na Mahakama iliendelea kusikiliza kesi hiyo kuanzia saa 3:30 asubuhi.

Post a Comment

0 Comments