By Arushadigital -Dar
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imekubaliana na pingamizi lililowekwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, dhidi ya shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri, ikieleza kuwa shahidi huyo hana sifa za kisheria kuwasilisha vielelezo vya video katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Lissu amewasilisha pingamizi manne, akipinga ushahidi wa Mkaguzi wa Polisi na Mtaalamu wa Uchunguzi wa Kielektroniki, Samwel Kaaya, kuhusu flash disk na kadi ya kumbukumbu (memory card) zinazodaiwa kuwa na picha za mjongeo.
Uamuzi huo umetolewa leo na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.
Jaji Ndunguru amesema hoja kuu iliyojadiliwa mahakamani ni iwapo shahidi huyo anastahili kuwasilisha ushahidi huo kama mtaalamu au la.
“Mshtakiwa aliwasilisha pingamizi akidai kuwa shahidi huyo si mtaalamu wa masuala ya video au teknolojia ya kielektroniki (cyber), bali ni mtaalamu wa picha aliyeteuliwa kwa mujibu wa GN 745 ya Desemba 16, 2022, iliyotolewa chini ya Kifungu cha 216 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA),” amesema Jaji Ndunguru.
Kwa mujibu wa hoja za Lissu, uteuzi wa shahidi huyo haukumruhusu kushughulika na vielelezo vya video, bali picha pekee, na zaidi hakuteuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kama mtaalamu wa video, hivyo hana mamlaka ya kuwasilisha ushahidi huo mahakamani.
Mshtakiwa alisisitiza kuwa video ni tofauti na picha zilizochapishwa, kwa hiyo shahidi huyo angehitajika kuwa na utaalamu maalum wa teknolojia ya kielektroniki ili kushughulikia vielelezo hivyo.
Kwa upande wa Jamhuri, walipinga pingamizi hilo wakieleza kuwa shahidi ana uwezo wa kitaalamu na ndiye aliyefanya uchunguzi na kuandaa ripoti ya vielelezo husika. Wamesisitiza kuwa video ni aina ya picha, hivyo tofauti kati ya viwili hivyo si kubwa katika muktadha wa ushahidi wa kitaalamu.
Hata hivyo, Mahakama ilifanya uchambuzi wa kina wa hoja hizo na kubaini kuwa Kifungu cha 216 cha CPA kinazungumzia picha (photographs) pekee na si picha za mjongeo (video).
Mahakama imeeleza kuwa video zina mahitaji maalum ya kiteknolojia na zinachukuliwa kama ushahidi wa kielektroniki, ambao unahitaji mtaalamu mwenye utaalamu maalum katika fani hiyo.
“Shahidi ambaye ni mtaalamu wa picha hana uwezo wa kisheria kushughulikia video zinazohifadhiwa kwenye flash au memory card. Uteuzi wake haukumruhusu kuhusika na video, bali picha tu. Hivyo, hawezi kuwa shahidi sahihi kwa ushahidi huu,” amefafanua Jaji Ndunguru.
Kutokana na hilo, Mahakama imekubaliana na pingamizi la Lissu na kusisitiza kuwa vielelezo hivyo havitakubaliwa kama ushahidi katika shauri hilo, ikisema hoja hiyo pekee inatosha kutupilia mbali ombi la Jamhuri la kuwasilisha vielelezo hivyo kupitia shahidi huyo.
Ends...

0 Comments