ZAIDI ya vijana 1,000 kutoka sharika 49 za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Arusha Mashariki wanatarajiwa kushiriki kwenye bonanza kubwa la michezo litakalofanyika Oktoba 14, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya kifo cha Mwasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumza na Arushadigital, Makamu Mwenyekiti wa Idara ya Vijana wa Jimbo hilo, Goodluck Sarakikya, alisema maandalizi yote yamekamilika na bonanza hilo litafanyika katika viwanja vya General Tyre, jijini Arusha.
“Tunawakaribisha vijana wote wa Jimbo la Arusha Mashariki kushiriki michezo mbalimbali kutoka kanda nne — Kanda ya Mlimani, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati na Kanda ya Tambarare. Itakuwa ni siku ya furaha, umoja na maonyesho ya vipaji,” alisema Sarakikya.
Alitaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni mpira wa miguu, netiboli, mbio, kuvuta kamba, kushindana kunywa soda na mingine mingi yenye lengo la kuburudisha, kujenga afya na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa vijana.
Kwa upande wake, Katibu wa Vijana wa Jimbo hilo, Godwin Twati, alisema bonanza hilo ni kilele cha tamasha la michezo lililokuwa likiendelea katika ngazi za kanda kwa muda wa wiki kadhaa.
“Lengo la bonanza hili ni kuwaunganisha vijana katika imani ya kanisa, kuwaimarisha kiafya na kuibua vipaji vipya kupitia michezo. Ni awamu ya tatu tangu kuanzishwa kwake, na limekuwa na matokeo makubwa katika kuwaandaa vijana kuwa viongozi wa kesho,” alisema Twati.
Aidha, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Engarenarok, Solomoni Dereva, alisema bonanza hilo limekuwa chachu ya umoja, upendo na mshikamano kwa vijana wa KKKT Arusha Mashariki.
“Kupitia michezo, vijana wetu wamejifunza kushirikiana, kuheshimiana na kudumisha amani. Tumeamua kufanya bonanza hili siku ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere kama njia ya kumuenzi kupitia michezo na uzalendo,” alisema Mchungaji Dereva.
Zaidi ya michezo na burudani, washindi wa mashindano mbalimbali watatunukiwa zawadi maalum, ikiwa ni sehemu ya motisha na kutambua jitihada zao katika kuonesha vipaji na nidhamu bora ya michezo.
Zawadi hizo zitahusisha vikombe, medali, jezi, vyeti vya ushindi pamoja na zawadi za heshima kwa timu na washiriki watakaofanya vizuri katika michezo yote.
Bonanza hilo linatarajiwa kuvutia mamia ya watazamaji na waumini kutoka maeneo mbalimbali ya Arusha, huku likiambatana na burudani, michezo ya ushindani, ibada fupi ya shukrani pamoja na matukio ya kijamii yanayolenga kujenga afya ya mwili na roho.
Kwa mujibu wa waandaaji, bonanza la vijana wa KKKT Arusha Mashariki limekuwa likikua mwaka hadi mwaka, na linatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo ya kijamii katika eneo hilo mwaka huu.
-Ends.....




0 Comments