KAMATI YA BUNGE YAELEKEZA UBORESHAJI ZAIDI BUSTANI YA THEMI, YATAKA ENEO MAALUMU LA VIONGOZI WAKUU (VIP)

 KAMATI YA BUNGE YAELEKEZA UBORESHAJI ZAIDI BUSTANI YA THEMI, YATAKA ENEO MAALUMU LA VIONGOZI WAKUU (VIP)

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeelekeza kuboreshwa zaidi kwa miundombinu ya Bustani ya Mapumziko ya Themi jijini Arusha, ikisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa eneo maalumu la kupumzikia viongozi wa ngazi za juu (VIP), ili kuendana na hadhi ya jiji hilo kama kitovu cha utalii na diplomasia nchini.

Maelekezo hayo yametolewa leo Machi 17, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Florent Kyombo, wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua maendeleo ya mradi wa uboreshaji wa bustani hiyo, unaotekelezwa katika Jiji la Arusha.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo,  Kyombo alisema kuwa pamoja na kuridhishwa na hatua ya utekelezaji wa mradi huo, bado kuna haja ya kuongeza thamani ya bustani hiyo kwa kujenga eneo maalumu litakaloweza kupokea viongozi wakuu wa kitaifa na kimataifa.

Alifafanua kuwa Arusha si tu lango la utalii wa kaskazini, bali pia ni jiji la kidiplomasia linalopokea wageni wa hadhi ya juu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo linapaswa kuwa na maeneo ya kisasa na yenye hadhi ya juu kwa ajili ya mapumziko na burudani.

“Kutokana na ugeni wa kidiplomasia hapa Arusha, ni muhimu bustani ya Themi iwe na eneo maalumu kwa ajili ya watu muhimu sana (VIP). Hapa ni mahali ambapo hata Mheshimiwa Rais anaweza kufika na wageni wake, wakiwemo marais wa nchi nyingine, kupumzika na kujionea vivutio vya utalii wa vyakula na mazingira ya mkoa huu,” alisisitiza Mhe. Kyombo.

Kwa upande wake, Kamati hiyo imeipongeza Serikali kwa kuanzisha mradi huo, ikieleza kuwa ni hatua muhimu katika kukuza sekta ya utalii wa ndani na nje, pamoja na kuboresha mandhari ya jiji la Arusha.

Wajumbe wa Kamati walibainisha kuwa uwepo wa bustani ya kisasa ya mapumziko utachangia kuongeza vivutio vya utalii, hasa kwa wageni wanaofika Arusha kwa shughuli za kikazi, mikutano ya kimataifa na matembezi.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, alisema kuwa mradi wa uboreshaji wa Bustani ya Themi unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3.

Alieleza kuwa fedha hizo zinatoka Serikali Kuu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, kupitia mpango wa kuboresha miji na majiji nchini (TACTIC), unaolenga kuinua hadhi ya maeneo ya mijini kwa kuzingatia mahitaji ya kisasa.

Kwa mujibu wa Kayombo, mradi huo unatekelezwa na kampuni ya M/S Mohamedi Building Ltd na hadi sasa umefikia asilimia 20.17 ya utekelezaji, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2026.

Mradi huo unalenga kuboresha miundombinu ya mapumziko, ikiwemo maeneo ya bustani, huduma za kijamii, pamoja na mazingira rafiki kwa wakazi na wageni, hatua inayotarajiwa kuifanya Arusha kuwa miongoni mwa majiji yenye vivutio bora vya mapumziko nchini.

Kwa ujumla, maelekezo ya Kamati hiyo yanatarajiwa kuongeza ubora na hadhi ya bustani hiyo, na kuifanya kuwa sehemu muhimu ya mapumziko, utalii na shughuli za kijamii kwa wakazi wa Arusha na wageni kutoka ndani na nje ya nchi.






Post a Comment

0 Comments