MGOGORO WA ‘WAZUNGU WA ARUSHA’ WATINGA MAHAKAMA KUU, WAKILI YOYO AFUNGUKA KILA KITU

  MGOGORO WA ‘WAZUNGU WA ARUSHA’ WATINGA MAHAKAMA KUU

Ugomvi wa ardhi ya ekari 10 wazua taharuki, walinzi wagombana eneo la uwekezaji

Na Joseph Ngilisho- ARUMERU


MGOGORO wa umiliki wa ardhi unaohusisha wawekezaji wa kigeni katika sekta ya utalii wilayani Arumeru mkoani Arusha, sasa umefika katika Mahakama Kuu huku ukianza kuchukua sura mpya ya taharuki kufuatia mvutano wa walinzi uliotokea mwishoni mwa wiki.

Wakili wa Mahakama Kuu na Mwanasheria wa Kampuni ya Ker & Downey Safaris Limited (KDT), Bw. Asubuhi Yoyo, amesema mgogoro huo unamhusisha mmiliki wa Kampuni ya Kigelia Africana Limited, Bw. George Hurtly, na unahusu umiliki wa eneo la takribani ekari 10.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Machi 17, 2026 wilayani Arumeru, Wakili Yoyo alisema chanzo cha mgogoro huo ni kuvunjwa kwa makubaliano ya awali ya mauziano ya ardhi kati ya pande hizo mbili.

Alifafanua kuwa Kampuni ya Kigelia, inayomilikiwa na raia huyo wa Marekani, awali iliingia makubaliano na KDT kununua ekari 10, lakini kwa masharti kuwa eneo lote la ekari 600 linalomilikiwa na KDT lipimwe kwanza na kugawanywa katika hati ndogo ndogo kabla ya umiliki kuhamishwa rasmi.

“Hata hivyo, hadi sasa zoezi la upimaji halijakamilika, jambo ambalo lilikuwa msingi wa utekelezaji wa makubaliano yale. Kutokana na hali hiyo, upande wa Kigelia ulivunja masharti ya mkataba na kuanza kuchukua hatua za umiliki bila kufuata taratibu za kisheria,” alisema Wakili Yoyo.

Kwa mujibu wa maelezo yake, kabla ya mgogoro huo,Hurtly aliwahi kuwa mfanyakazi wa KDT kwa muda mrefu na baadaye aliuziwa ekari 22 bila kuwepo kwa mgogoro wowote.




“Mauziano ya awali ya ekari 22 yalienda vizuri kabisa na hayana mgogoro. Tatizo limejitokeza kwenye makubaliano mapya ya ekari 10 yaliyofanyika mwaka 2023/2024,” alisisitiza.

Wakili huyo alidai kuwa baada ya kuvunjika kwa makubaliano, Kampuni ya KDT ilichukua hatua ya kusitisha mkataba huo na kumrejeshea mnunuzi fedha kiasi cha dola za Marekani 15,000 alizokuwa amelipa kama sehemu ya makubaliano.

Aidha, alieleza kuwa licha ya kurejeshewa fedha hizo, upande wa Kigelia ulidai umiliki wa eneo hilo na kuanza kulichukua kwa nguvu, ikiwa ni pamoja na kujenga uzio na kuonyesha nia ya kuanzisha hifadhi ndogo ya wanyama (zoo) ndani ya eneo hilo.

Mvutano huo ulifikia hatua mpya mwishoni mwa wiki baada ya Kampuni ya Kigelia kuleta walinzi wapya katika eneo hilo, hatua iliyosababisha mgongano na walinzi waliokuwa wakilinda eneo hilo kwa niaba ya KDT tangu mwaka 2009.

“Kilichotokea ni mvutano kati ya walinzi waliokuwepo na walinzi wapya walioletwa na upande wa Kigelia, kila mmoja akidai kulinda eneo hilo. Hali hiyo ilisababisha Jeshi la Polisi kufika eneo la tukio Ijumaa jioni na kudhibiti hali ya usalama,” aliongeza.

Kwa sasa, mgogoro huo unaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu, huku kila upande ukisisitiza haki yake ya umiliki wa ardhi hiyo yenye thamani kubwa katika sekta ya utalii.

Tukio hilo linaibua maswali mapana kuhusu usimamizi wa mikataba ya uwekezaji na umiliki wa ardhi nchini, hasa katika maeneo yenye mvuto wa kitalii kama Arusha, ambapo migogoro ya aina hiyo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.

Ends..

Post a Comment

0 Comments