UHITAJI WA STENDI MPYA WAIBUA MAPINDUZI ARUSHA: KAMATI YA BUNGE YAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA “TABASAMU” LA WANANCHI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Kwa miaka mingi, Jiji la Arusha limekuwa likikabiliwa na changamoto ya uhaba wa kituo cha kisasa cha mabasi yaendayo mikoani—hali iliyokuwa ikiathiri hadhi ya jiji hilo kama kitovu cha utalii na biashara nchini. Hata hivyo, sasa matumaini mapya yameibuka kufuatia ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Mabasi cha Bondeni (Bondeni City Bus Terminal), mradi unaotajwa kuwa suluhisho la muda mrefu kwa tatizo hilo.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua hiyo waliyoieleza kuwa ni “tabasamu” kwa wananchi wa Arusha waliokuwa na kiu ya muda mrefu ya kuwa na stendi ya kisasa.
Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 17, 2026, baada ya wajumbe hao kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kuridhishwa na kiwango cha utekelezaji wake, pamoja na ubora wa miundombinu inayojengwa.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Floreny Kyombo, alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za usafiri na kukuza uchumi wa jiji hilo.
“Tunafahamu Arusha ni lango la utalii na hupokea wageni wengi wa ndani na nje ya nchi kila siku. Ujenzi wa stendi hii ya kisasa unaendana na hadhi ya jiji hili. Tunampongeza sana Mhe. Rais kwa kuwaletea wanaArusha tabasamu hili,” alisema Kyombo.
Aliongeza kuwa, kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakihitaji kituo chenye hadhi ya kimataifa kitakachorahisisha usafiri na kuboresha mazingira ya wafanyabiashara pamoja na wasafiri.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Lucy Mwakyembe (Mb), alisema Serikali imeonyesha nia ya dhati kwa kutoa fedha nyingi kuhakikisha Arusha inapata stendi ya kisasa inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
“Mradi huu unaonesha jinsi Serikali inavyothamini nafasi ya Arusha kama mji wa kimataifa wa utalii. Hii siyo tu stendi, bali ni alama ya maendeleo na ustaarabu wa jiji,” alisema Mwakyembe.
Naye Mhe. Abdalah Chaurembo alipongeza usanifu wa kituo hicho, akibainisha kuwa kimezingatia mahitaji muhimu ya watumiaji wote, ikiwemo uwepo wa maeneo ya ibada na huduma nyingine za kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, John Kayombo, alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 14.3, fedha zinazotolewa na Benki ya Dunia kupitia programu ya TACTIC.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri, kuongeza mapato ya jiji na kuboresha taswira ya Arusha kitaifa na kimataifa.
Ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Bondeni unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa eneo hilo, huku ukitoa ajira na fursa za biashara kwa wakazi wa jiji hilo.
Ends .



0 Comments