KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UJENZI WA SOKO LA KILOMBERO ARUSHA, YASIFIA VIWANGO VYAKE
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Soko la Kilombero katika Jiji la Arusha, ikieleza kuwa kukamilika kwake kutaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya biashara na ustawi wa wafanyabiashara wa eneo hilo.
Wajumbe wa kamati hiyo walitembelea na kukagua mradi huo leo Machi 17, 2026, ambapo walibaini kuwa ujenzi unaendelea kwa kasi na umezingatia viwango vinavyotarajiwa, hali inayotoa matumaini ya kuboresha mazingira ya biashara ukilinganisha na hali ilivyokuwa awali.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Florent Kyombo (Mb), aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya masoko ya kisasa nchini. Alieleza kuwa soko hilo litachochea ukuaji wa uchumi wa Jiji la Arusha kwa kuwapatia wafanyabiashara sehemu salama, yenye hadhi na rafiki kwa shughuli zao.
Alisema masoko ya kisasa kama la Kilombero si tu yanapandisha hadhi ya miji, bali pia yanahakikisha usalama wa wafanyabiashara na wateja, sambamba na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha, Mhe. Kyombo aliwataka wananchi wa mkoa wa Arusha kuendelea kumuunga mkono Rais na juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wao.
“Niwaombe wananchi, hususan wafanyabiashara, kuendelea kushirikiana na viongozi wa ngazi zote. Lengo ni kuhakikisha mnapata huduma bora na kunufaika na fursa zilizopo,” alisema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Charles Mahera (Mb), alibainisha kuwa miundombinu ya soko hilo imezingatia viwango vya kisasa na kimataifa, ikijumuisha huduma muhimu za kijamii kama vyumba maalum vya kupumzikia na kunyonyeshea watoto kwa kina mama.
Alieleza kuwa uwepo wa huduma hizo utasaidia kuboresha afya na ustawi wa watoto, hasa wale wa chini ya miaka mitano, kwa kuwa karibu na mama zao wakati wa shughuli za biashara, hatua itakayochangia pia kupunguza changamoto za lishe duni.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa kamati hiyo waliupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, wakisema utekelezaji wa mradi huo unaonesha ushirikiano thabiti kati ya viongozi wa ngazi mbalimbali za Serikali.
Kwa ujumla, Kamati hiyo imeeleza matumaini yake kuwa kukamilika kwa Soko la Kilombero kutakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa Arusha na maeneo jirani, huku likiwa mfano wa utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi.





0 Comments