MWEKEZAJI WA KIGENI ADAI KUFUNGIWA NDANI NA ASKARI WENYE SILAHA ARUMERU
Mgogoro wa uwekezaji watikisa sekta ya utalii, walinzi binafsi waondolewa na kuwekwa wengine
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
KATIKA tukio lisilo la kawaida lililozua maswali mengi kuhusu usalama wa wawekezaji nchini, mwekezaji wa kigeni wa kampuni ya utalii ya Kigelia Africana Limited, George Heartely, anadaiwa kuzuiwa nyumbani kwake chini ya ulinzi mkali na askari wanaodaiwa kuwa polisi wenye silaha za moto wakishirikiana na kampuni binafsi ya ulinzi, ambao walimzuia kutoka ndani ya makazi yake yaliyopo eneo la Olorieni wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, askari hao wanaodaiwa kutoka Wilaya ya Arumeru waliwasili katika eneo hilo usiku wa kuamkia jana bila kujitambulisha rasmi kwa mwekezaji huyo huku video cha ulinzi za CCTV zikiwaonesha. Inadaiwa walimuwekea ulinzi mkali na kumzuia kutoka nje ya nyumba yake kuanzia usiku hadi majira ya saa tano asubuhi ya leo.
Taarifa zinaeleza kuwa hali hiyo ilitokea wakati askari hao wakifanya operesheni ya kuwaondoa walinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Bonds Security, waliokuwa wakilinda eneo la uwekezaji la kampuni hiyo.
Baada ya kuwaondoa walinzi hao, askari hao waliwapeleka katika kituo cha polisi kwa mahojiano, ambapo hadi sasa wanadaiwa kushikiliwa katika kituo hicho. Kufuatia hatua hiyo, inaelezwa kuwa askari hao waliweka kampuni nyingine ya ulinzi binafsi kuchukua jukumu la kulinda eneo hilo.
Uwekezaji wa hoteli na bustani ya wanyama
Mwekezaji huyo,George Heartely, amewekeza katika mradi wa hoteli ya kitalii pamoja na bustani ya kuhifadhi wanyama (Zoo) katika eneo hilo, ndani ya ardhi inayokadiriwa kuwa na ukubwa wa ekari 43.Mradi huo pia unaelezwa kuhusisha shughuli za uhifadhi wa wanyamapori kwa mfumo wa Wildlife Management Area (WMA), mfumo unaosimamiwa na jamii kwa lengo la kulinda na kuhifadhi rasilimali za wanyamapori huku ukiwanufaisha wananchi wa maeneo husika.
Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali zinazodaiwa kutolewa na Serikali, mwekezaji huyo anamiliki kisheria eneo hilo na ameajiri kampuni ya Bonds Security kulinda mali na miundombinu ya uwekezaji wake.
Chanzo cha mgogoro
Chanzo cha tukio hilo kinatajwa kuwa ni mgogoro wa kibiashara unaodaiwa kutokea kati ya kampuni ya Kigelia Africana Limited inayomilikiwa na Heartely na kampuni nyingine ya uwekezaji ya kigeni inayojulikana kama KDT, ambayo ina mradi wa uwekezaji jirani na eneo hilo.
Akizungumzia sakata hilo, Wakili wa kampuni ya Bonds Security, John Severine, alisema mgogoro huo unatokana na suala la njia ya kupita inayodaiwa kuunganisha lango la kampuni ya Kigelia Africana Limited kuelekea katika eneo la kampuni ya KDT.
Kwa mujibu wa wakili huyo, mwekezaji wa Kigelia Africana aliamua kujenga uzio katika eneo lake ili kudhibiti usalama wa mradi huo pamoja na kuzuia wanyama anaowahifadhi kutoroka nje ya eneo hilo.
“Eneo hilo linamilikiwa kisheria na kampuni ya Kigelia Africana Limited kwa mujibu wa hati ya miliki waliyopewa na Serikali, na ujenzi wa uzio ulikuwa ni sehemu ya hatua za kulinda uwekezaji huo,” alisema.
Sintofahamu ya vibali vya ujenzi
Taarifa zinaonyesha kuwa mwekezaji huyo alipata kibali cha ujenzi wa uzio Machi 9, 2026 kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Hata hivyo, katika hali iliyozua sintofahamu, inadaiwa kuwa siku ya Jumapili Machi 15, 2026 — siku ambayo si ya kazi serikalini — ofisi hiyo hiyo ya Mkurugenzi ilitoa barua ya kusitisha ujenzi huo, ikidai kuwa kampuni hiyo haina kibali halali cha kuendelea na ujenzi huo.
Hatua hiyo imeibua maswali kutokana na ukweli kwamba barua ya kusitisha ujenzi haikuweka wazi iwapo ofisi hiyo inatambua au inapinga kibali cha ujenzi kilichotolewa siku tano kabla.
Serikali ya mtaa iliarifiwa
Kwa mujibu wa taarifa za upande wa mwekezaji, tayari walikuwa wamemjulisha Afisa Mtendaji wa Kata ya Olorieni kuhusu mpango wa ujenzi huo.
Inaelezwa kuwa tarehe 4 Machi 2026 mwekezaji huyo aliwasilisha taarifa rasmi kuwa kutakuwa na ujenzi wa uzio katika eneo lake na kwamba barabara ndogo inayokatiza katika shamba hilo ingefungwa kwa muda kwa ajili ya shughuli za ujenzi.
Taarifa hiyo inadaiwa kupokelewa na Afisa Mtendaji wa Kata hiyo ambaye aliridhia na kuthibitisha kuwa ofisi yake imepokea taarifa hiyo.
Ujenzi huo ulianza rasmi Machi 11, 2026 kabla ya kuzuiwa ghafla Jumapili Machi 15, 2026.
Historia ya uwekezaji
Mshauri wa kampuni ya Kigelia Africana Limited, David Bulengo, alieleza kuwa awali George Heartely alikuwa mfanyakazi wa kampuni ya KDT kabla ya kusimamishwa kazi.
Baadaye aliamua kuanzisha uwekezaji wake binafsi nchini Tanzania kwa kuanzisha mradi wa utalii katika eneo hilo la Arusha.
Bulengo alisema awali kampuni ya KDT ilimuuzia Heartely eneo la ekari 10, ambalo baadaye aliliongeza kwa kununua maeneo mengine hadi kufikia ekari 43.
Hata hivyo, alidai kuwa tofauti kati ya wawekezaji hao zilianza kujitokeza baada ya kugundua kuwa kampuni ya Kigelia Africana Limited inaendesha uwekezaji wa aina inayofanana na ule wa kampuni ya KDT.
Mkuu wa wilaya azungumzia sakata hilo
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Mwinyi, alisema tayari amesikia taarifa za mgogoro huo ingawa bado haujawasilishwa rasmi katika ofisi yake na linashughulikiwa ngazi ya mkoa ,hata hivyo jitihada za kumpata mkuu wa Mkoa wa Arusha Amos Makala ama Katibu Tawala , Dkt Toba Nguvila bado zinaendelea.
“Nimesikia kuhusu sakata hilo, lakini bado halijafika rasmi ofisini kwangu kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema.
Sakata hilo linaibua mjadala mpana kuhusu ulinzi wa uwekezaji na utatuzi wa migogoro ya kibiashara, hasa katika sekta ya utalii ambayo ni moja ya nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania.
Ends











0 Comments