BABA ARUSHA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUWABAKA WATOTO WAKE WAWILI, MMOJA AKIWA NA MIEZI SITA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Mkazi wa eneo la Oloirien jijini Arusha, Hamis Ramadhani (38), anashikiliwa na vyombo vya dola kufuatia tuhuma nzito za kuwabaka watoto wake wawili wa kike, mmoja akiwa na umri wa miezi sita na mwingine miaka sita.
Taarifa kutoka kwa majirani wa familia hiyo zinaeleza kuwa tukio hilo lilifichuka baada ya mke wa mtuhumiwa, Zanura Rashidi, pamoja na majirani kugundua mwenendo usio wa kawaida ndani ya familia hiyo, hali iliyosababisha uchunguzi wa haraka na hatimaye kumuweka mtuhumiwa chini ya ulinzi wa wananchi kabla ya kukabidhiwa kwa polisi.
Kwa mujibu wa majirani, matukio hayo hayakuwa ya siku moja bali yalikuwa yakijirudia mara kwa mara, hasa wakati mtuhumiwa anapokuwa amelewa pombe.
Inaelezwa kuwa katika nyakati hizo mtuhumiwa alikuwa akimfukuza mkewe nje ya nyumba na kumlazimisha kulala nje, hali iliyompa nafasi ya kutekeleza vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya watoto wake.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa baada ya tetesi za vitendo hivyo kusambaa mtaani, wananchi walimfuata mtuhumiwa katika kijiwe chake cha kawaida kabla ya kumuweka chini ya ulinzi wao wakisubiri hatua za kisheria.
Mtuhumiwa huyo, ambaye ni dereva wa bodaboda katika eneo hilo, alidaiwa kukiri kuhusika na vitendo hivyo wakati akihojiwa na wananchi waliomzingira kabla ya kufikishwa kituo cha polisi.
Katika maelezo yake, alidai kuwa amekuwa akifanya vitendo hivyo mara kwa mara kwa mtoto wa miaka sita, akitoa kauli iliyozua hasira na mshangao kwa wananchi waliokuwepo eneo hilo.
Kwa upande wake, mama wa watoto hao, Zanura Rashidi, alisema tukio lililofichua ukweli lilitokea baada ya mumewe kurejea nyumbani akiwa amelewa na kumpatia fedha kiasi cha shilingi 4,000 ili aende kununua nyama buchani.
Alisema aliporejea nyumbani, mtoto wake mkubwa mwenye umri wa miaka 11 alimuita pembeni na kumueleza kuwa usiku uliopita baba yao alimbaka mtoto wa miezi sita huku akimtaka mtoto mwingine mwenye miaka sita kufumba macho wakati akitekeleza kitendo hicho.
Mama huyo aliongeza kuwa baada ya kumaliza kitendo hicho, mtuhumiwa alidaiwa kumfuta mtoto huyo sehemu za siri kabla ya kuondoka.
Baada ya taarifa hizo kusambaa, wananchi walijikusanya kwa hasira na kuamua kumtafuta mtuhumiwa ili achukuliwe hatua za kisheria.
Mtuhumiwa kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria, huku wananchi wa eneo hilo wakilaani vikali tukio hilo na kuomba sheria ichukue mkondo wake ili haki ipatikane kwa watoto hao.
Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa katika jamii kuhusu umuhimu wa kulinda haki za watoto na kutoa taarifa mapema pindi vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinapobainika.

0 Comments