JESHI LA POLISI LATOA TAMKO KUPOTEA KWA PADRI NIKATA

 By Arushadigital-RUVUMA


JESHI la Polisi Mkoa wa Ruvuma linaendelea na uchunguzi wa tukio la kupotea kwa Padre Camillus Nikata, wa Jimbo Kuu la Songea, ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Mwanza.


Akizungumza na vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G. Chilya, amesema Padri Nikata alifika Songea tarehe 03, Oktoba 2025 akitokea Dodoma, akiwa na mhadhiri mwenzake ambaye pia ni Padre wa Jimbo la Songea, na kufikia katika nyumba ya Mapadre St. Shanney.


Taarifa zinaeleza kuwa mnamo tarehe 07, Oktoba 2025, majira ya jioni, Padre Nikata alionekana kwa mara ya mwisho na Padre mwenzake katika Mtaa wa Kanisani, akiwa na kibegi kidogo mkononi akielekea Stendi ya zamani ya Mabasi Mfaranyaki. Tangu siku hiyo, hajarejea alipokuwa amefikia.


Baada ya jitihada za kumtafuta katika maeneo mbalimbali kukosa mafanikio, tarehe 09 Oktoba 2025 Kanisa na Mapadre wenzake walitoa taarifa rasmi kwa Polisi kuhusu kutoweka kwake. Jeshi la Polisi limeendelea na uchunguzi kubaini alipo Padre Nikata na mazingira ya kupotea kwake.


Post a Comment

0 Comments