PADRI KATOLIKI ATOWEKA GHAFLA KANISA LINAMTAFUTA

 UJUMBE KUTOKA KWA ASKOFU MKUU WA SONGEA 

TAARIFA YA KUTOONEKANA KWA PADRE CAMILLUS NIKATA


Kwa niaba ya wanajimbo Kuu la Songea tunapenda kutoa taarifa kwamba Mheshimiwa Padre Camillus Nikata wa Jimbo Kuu la Songea, ambaye ni Mhadhili katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Mwanza, haonekani wala hapatikani kwenye simu yake.  


Padre Nikata alikuwa ametokea Dodoma kwenye mafundisho ya moyo ya mapadre wanaofundisha katika Vyuo vikuu vya TEC, akiwa na mhadhili mwenzake, ambaye ni Padre wa Jimbo hili. Hapa Songea alikaa katika nyumba ya mapadre, St. Vianney. Alikuwa amepanga kusafiri kwenda Mwanza tarehe 08 Oktoba 2025, siku ya Jumatano asubuhi, kwa basi la SUPERFEO, na tiketi alishainunua kwa mtandao. Lakini siku hiyo ya Jumatano mchana tulianza kuhisi kwamba hajasafiri kwenda Mwanza kwani katika chumba chake kilichokuwa kimefungwa ilionekana mizigo yake ambayo alikuwa ameiandaa kwa ajili ya safari. Mtumishi wa nyumba ya mapadre alishangaa kwamba mzigo ambao Padre ilitakiwa auchukue toka kwake haukuchukuliwa. Pia mlango wa chumba ulifungwa, lakini ufunguo haukurudishwa kwa mtumishi.


Baada ya kuona hayo tulianza kumtafuta kwa simu na kwa kuulizia kwa watu aliokaa nao katika nyumba ya mapadre. Hata hivyo hatukufaulu kupata chochote, maana hakupatikana kwa simu na watu hawakujua alikokwenda. Kule Mwanza alikotakiwa kwenda, nako haonekani na hapatikani. Ofisi ya SUPERFEO ilidhihirisha kuwa Padre Nikata alinunua tiketi lakini hakusafiri kwa basi lile.


Baada ya kushindikana kwa jitihada za kumtafuta kila mahali ambapo tulidhani angeweza kuwepo, tumepeleka taarifa Polisi.


Imetolewa na

 Damian Dallu

ASKOFU MKUU,SONGEA

Post a Comment

0 Comments