SAKATA LA WAZUNGU LAINGIA HATUA MPYA, SERIKALI YATINGA, YASITISHA HATI YA ARDHI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SAKATA la mgogoro wa kibiashara unaowahusisha raia wa kigeni (maarufu kama “Wazungu”) hapa nchini limechukua sura mpya, kufuatia Serikali ya Mkoa wa Arusha kuingilia kati na kuchukua hatua ya kusitisha hati ya umiliki wa ardhi ya mwekezaji aliyedai kuzuiwa kuingia katika eneo lake.
Hatua hiyo imekuja baada ya mvutano mkali wa umiliki wa ardhi unaowahusisha wawekezaji kutoka Marekani wanaojihusisha na shughuli za utalii wilayani Arumeru, mgogoro ambao umeibua taharuki na kuvuta hisia za wadau wa uwekezaji na umma kwa ujumla.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Serikali ya Mkoa imeamua kusitisha hati ya umiliki wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 10.58 iliyokuwa imetolewa kwa mwekezaji George Hurtly, mmiliki wa kampuni ya Kigelia Africana Limited, baada ya kubainika kuwa ilitolewa kimakosa huku kukiwa na shauri linaloendelea mahakamani kuhusu umiliki wa eneo hilo.
Uamuzi huo ulifikiwa baada ya kikao cha pamoja kati ya pande zote mbili zinazohusika katika mgogoro huo, kilichosimamiwa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Arusha, ambapo uchunguzi wa awali ulibaini kuwa taratibu za utoaji wa hati hazikuzingatia uwepo wa mgogoro wa kisheria uliokuwa tayari umefikishwa mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Arusha, Frank Minzikuntwe, alithibitisha hatua hiyo na kueleza kuwa serikali imechukua uamuzi huo kwa lengo la kulinda misingi ya sheria na kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.
“Kwa sasa siwezi kulizungumzia jambo hili kwa kina hadi nipate kibali kutoka kwa Katibu Mkuu, lakini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itatoa ufafanuzi kamili mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi,” alisema Minzikuntwe.
Aliongeza kuwa ofisi yake tayari imefanya ziara katika eneo husika kwa ajili ya uhakiki wa mipaka na vielelezo vya umiliki, pamoja na kusikiliza hoja za kila upande ili kupata taswira halisi ya mgogoro huo.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Kampuni ya Ker & Downey Safaris Limited (KDT), Wakili Asubuhi Yoyo, alisema hatua ya kusitishwa kwa hati hiyo ni ushahidi kuwa mchakato wa kisheria umeanza kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
Alifafanua kuwa hati hiyo ilitolewa mwezi Februari mwaka huu baada ya mwekezaji huyo kuwasilisha nyaraka katika idara za ardhi bila kuweka wazi kuwa kulikuwa na shauri mahakamani kuhusu eneo hilo, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kisheria.
“Kusitishwa kwa hati hiyo kunamaanisha madai yaliyotolewa kuwa mwekezaji huyo amezuiwa kuingia katika eneo lake hayana msingi wa kisheria, kwani suala hilo tayari lipo mahakamani na linaendelea kushughulikiwa,” alisema Wakili Yoyo.
Akizungumzia tukio la mwishoni mwa wiki lililoibua mjadala mkubwa, Wakili huyo alikanusha madai ya kuzuiwa kwa mwekezaji huyo kuingia katika eneo lake, akieleza kuwa walinzi wa kampuni ya Kigelia ndio walizuiwa baada ya kuingia katika eneo la KDT na kuanza kujenga uzio uliolenga kufunga barabara ya matumizi ya pamoja.
Alisema hatua hiyo ililazimisha kampuni yao kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ambao walifika katika eneo hilo na kuwaondoa walinzi hao, huku Halmashauri ya Arusha DC ikiwa tayari imetoa zuio la shughuli za ujenzi katika eneo hilo hadi mgogoro utakapopatiwa ufumbuzi wa kisheria.
Kwa mujibu wa maelezo ya Wakili Yoyo, chanzo cha mgogoro huo kinatokana na makubaliano ya mauziano ya ardhi kati ya Kampuni ya KDT na Kigelia Africana Limited.
Alieleza kuwa awali mwekezaji huyo alinunua ekari 22 kutoka KDT bila kuwepo kwa tatizo lolote, na tayari ameendeleza uwekezaji wake kwa kujenga hoteli inayofanya kazi katika eneo hilo bila changamoto.
Hata hivyo, mgogoro ulianza katika makubaliano mapya ya ununuzi wa ekari 10 yaliyofanyika mwaka 2023/2024, ambapo kulikuwa na masharti maalum ya kisheria ambayo hayakufuatwa.
Alibainisha kuwa makubaliano hayo yalitaka eneo lote la ekari 600 linalomilikiwa na KDT lipimwe na kugawanywa katika hati ndogo ndogo kabla ya kuhamisha umiliki rasmi, lakini hadi sasa zoezi hilo halijakamilika.
“Licha ya masharti hayo kuwa wazi, upande wa Kigelia ulianza kuchukua hatua za umiliki kabla ya kukamilika kwa taratibu, jambo ambalo ni ukiukwaji wa mkataba,” alisisitiza.
Kutokana na hali hiyo, kampuni ya KDT ilichukua hatua ya kusitisha mkataba huo na kumrejeshea mwekezaji huyo kiasi cha dola za Marekani 15,000 alichokuwa amelipa kama sehemu ya malipo ya awali.
Hata hivyo, licha ya kurejeshewa fedha hizo, upande wa Kigelia uliendelea kudai umiliki wa eneo hilo na kuanza kuchukua hatua za kulimiliki kwa nguvu, ikiwemo kujenga uzio na kuonyesha nia ya kuanzisha hifadhi ndogo ya wanyama (zoo) ndani ya eneo hilo.
Mvutano huo ulifikia kilele mwishoni mwa wiki baada ya kampuni hiyo kupeleka walinzi wapya katika eneo hilo, hatua iliyosababisha mgongano na walinzi waliokuwa wakilinda eneo hilo kwa niaba ya KDT tangu mwaka 2009.
Akizungumza katika eneo la mgogoro baada ya ukaguzi wa mipaka, mwekezaji George Hurtly alisema ana imani kuwa serikali itachukua hatua stahiki na kuhakikisha haki inatendeka, huku akisisitiza kuwa tayari amepeleka shauri lake mahakamani.
“Kwa sasa hatuna cha ziada kusema, kwa kuwa suala hili liko mahakamani. Tunaamini haki itapatikana kupitia vyombo vya sheria,” alisema.
Wakati huo huo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu sakata hilo, akiahidi kuwa taarifa rasmi na hatua zitakazochukuliwa zitatolewa kwa umma kadri mchakato wa uchunguzi na kisheria unavyoendelea.
Sakata hilo linaendelea kuwa gumzo katika sekta ya uwekezaji na utalii, huku likizua mjadala mpana kuhusu uzingatiaji wa mikataba, uhalali wa hati za ardhi na umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria ili kuepusha migogoro inayoweza kuathiri mazingira ya uwekezaji nchini.
MWISHO




0 Comments