ZIARA YA KAMATI YA MICHEZO ARUSHA MJINI YAJENGA IMANI KUELEKEA UCHAGUZI WA SOKA
Na Joseph Ngilisho| ARUSHA
Kamati ya Michezo ya Wilaya ya Arusha Mjini imefanya ziara maalum ya kikazi kwa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Soka Wilaya ya Arusha Mjini (ADFA), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufuatilia na kujiridhisha na maandalizi ya uchaguzi wa viongozi wa soka unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu.
Ziara hiyo ililenga kupata taarifa za kina kuhusu mwenendo wa mchakato wa uchaguzi huo, hatua zilizofikiwa hadi sasa, pamoja na taratibu zinazofuatwa ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na kuzingatia kanuni za michezo.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa Kamati ya Michezo walipata fursa ya kuzungumza na Kamati ya Uchaguzi ya ADFA, ambapo waliwasilishwa taarifa ya hatua mbalimbali zilizotekelezwa, ikiwemo uandikishaji wa wagombea, maandalizi ya ratiba ya uchaguzi pamoja na mikakati ya kuhakikisha ushiriki mpana wa wadau wa soka katika wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa viongozi wa Kamati ya Michezo, walieleza kuridhishwa na namna kamati ya uchaguzi inavyotekeleza majukumu yake kwa umakini na uwajibikaji, wakisisitiza kuwa mchakato huo unaonesha dalili njema ya kupatikana kwa viongozi bora watakaosaidia kukuza soka la wilaya ya Arusha Mjini.
“Tumefurahishwa na maandalizi tuliyoyakuta hapa. Ni wazi kuwa kamati ya uchaguzi imejipanga vyema kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Aidha, Kamati ya Michezo iliahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa Kamati ya Uchaguzi ya ADFA ili kuhakikisha mchakato mzima unakamilika kwa mafanikio, huku wakitoa wito kwa wadau wote wa michezo kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwa kuzingatia amani na mshikamano.
Kwa upande wao, Kamati ya Uchaguzi ya ADFA ilishukuru kwa ziara hiyo, ikieleza kuwa ni chachu ya kuongeza uwajibikaji na kuimarisha imani kwa wadau wa soka. Walisisitiza dhamira yao ya kusimamia uchaguzi kwa misingi ya haki, uwazi na kufuata katiba pamoja na kanuni za chama.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa viongozi hao kupiga picha ya pamoja, ishara ya mshikamano na ushirikiano unaolenga kuinua maendeleo ya soka katika Wilaya ya Arusha Mjini.
Ends

0 Comments