SAMIA AVAA VIATU VYA MAGUFULI – TWARIQA YATOA TAFAKURI MIAKA MITANO BAADA YA KIFO CHAKE

 SAMIA AVAA VIATU VYA MAGUFULI – TWARIQA YATOA TAFAKURI MIAKA MITANO BAADA YA KIFO CHAKE

Na Joseph Ngilisho | Arusha

Katibu Mkuu wa Twariqa Taifa, Sheikh Haruna Husein, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha uongozi wenye mwendelezo kwa kufanikisha na kusimamia miradi mikubwa ya kimkakati iliyoachwa na mtangulizi wake, Hayati John Pombe Magufuli.

Sheikh Husein alitoa kauli hiyo leo Machi 19, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Twariqa, Zawia Kuu jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya tafakuri ya miaka mitano tangu kifo cha kiongozi huyo pamoja na kuelekea kilele cha maadhimisho ya Eid al-Fitr kinachotarajiwa kufanyika kesho kutwa.

Alisema kuwa Hayati Magufuli aliacha alama kubwa katika ujenzi wa taifa kwa kuanzisha na kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo reli ya kisasa (SGR) na mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere, ambayo ilikuwa imefikia hatua za juu za utekelezaji kabla ya kifo chake.

“Ni ukweli usiopingika kwamba miradi mingi aliacha ikiwa imekamilika au imefikia zaidi ya asilimia 90. Hili linaonesha namna alivyojitoa kwa dhati kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” alisema Sheikh Husein.

Aliongeza kuwa uongozi wa Rais Samia umefanikiwa “kuvaa viatu” vya mtangulizi wake kwa kuhakikisha miradi hiyo haikwami, bali inakamilika na kuanza kuwanufaisha wananchi, jambo alilolitaja kuwa ni ishara ya uongozi wenye busara na uzalendo.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna haja ya kuimarisha baadhi ya sekta ikiwemo utalii, hasa katika kuboresha miundombinu ya makumbusho na maeneo ya vivutio ili kuongeza thamani ya historia na elimu kwa wageni.

Aidha, alihimiza kuendelea kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya na miundombinu ya barabara ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote kwa usawa.

Katika nasaha zake kwa Watanzania kuelekea sikukuu ya Idd, Sheikh Husein alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na kuwaombea viongozi wa taifa.

“Katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuelekea Idd, ni wajibu wetu kumuombea kiongozi wetu na taifa letu kwa ujumla. Umoja na amani ndio msingi wa maendeleo ya kweli,” alisisitiza.

Alimalizia kwa kusema kuwa tofauti za mitazamo ya kiuongozi kati ya viongozi hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko, bali ziwe fursa ya kujifunza na kusonga mbele kama taifa moja lenye malengo ya pamoja.

Ends..

Post a Comment

0 Comments