TWARIQA WATOA WITO: ‘IDDI IWE MWANZO WA MAADILI, AMANI NA UMOJA WA TAIFA’
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
KATIBU Mkuu wa Taasisi ya Twariqa Tanzania, Sheikh Haruna Huseni, amewataka Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuifanya Sikukuu ya Eid al-Fitr kuwa mwanzo wa kudumisha maadili mema, kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kulinda amani ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Zawia Kuu jijini Arusha kuelekea mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadan, Sheikh Huseni alisema kuwa kipindi cha Ramadhani kimekuwa shule ya mafunzo ya maadili, hivyo ni wajibu wa kila Muumini kuyaendeleza hata baada ya mfungo kumalizika.Alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajaalia Waislamu kufika katika siku za mwisho za Ramadhani, akiwatakia kheri Waislamu wote duniani na Watanzania kwa ujumla, pamoja na Wakristo walioko katika kipindi cha Lent.
“Mwenyezi Mungu azikubali ibada zetu, atusamehe madhambi yetu na atujibu dua zetu,” alisema.
Dua Maalum kwa Taifa na Viongozi
Katika ujumbe wake, Sheikh Huseni alitoa wito kwa Waislamu kutumia mkusanyiko wa Swala ya Iddi kuombea taifa liendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano.
Alisisitiza kuwa dua hizo ziwe za dhati, zikitokana na unyenyekevu wa moyo baada ya kipindi cha siku 30 za ibada na kujizuia na maovu.
Aidha, aliwataka waumini kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ili apewe hekima, busara na nguvu ya kuiongoza nchi kwa haki na uadilifu.
Maadili ya Ramadhani Yaendelee
Akizungumzia mafunzo ya Ramadhani, Sheikh Huseni alisema mwezi huo umejenga misingi ya subira, upendo, uvumilivu na kusameheana—mambo ambayo ni nguzo ya jamii bora.
“Tusirudi katika matendo maovu mara tu baada ya Ramadhani. Tuendelee na moyo ule ule wa kusaidiana, kupendana na kusameheana,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa jamii itakayoshikamana na maadili hayo itakuwa na uwezo wa kujenga taifa lenye mshikamano na maendeleo endelevu.
‘Amani Kwanza’—Twariqa Yasisitiza
Kwa upande wa amani, Katibu Mkuu huyo alisema Taasisi ya Twariqa inaendelea kusimamia kauli mbiu ya “Amani Kwanza,” akisisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuilinda amani hiyo kwa gharama yoyote.
Aliwataka wananchi kuonesha uzalendo kwa vitendo kwa kulinda rasilimali za taifa ikiwemo hifadhi za wanyama na Mlima Kilimanjaro, akibainisha kuwa uchumi wa nchi unategemea kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii.
Vilevile, alihimiza busara katika mijadala ya kijamii na kisiasa ili tofauti za mawazo zisiwe chanzo cha migogoro bali ziwe daraja la kujenga taifa imara.
Maandalizi ya Iddi
Akihitimisha, Sheikh Huseni aliwatakia Waislamu wote na Watanzania kwa ujumla maandalizi mema ya Iddi, akisisitiza umuhimu wa kusherehekea kwa amani, furaha na mshikamano.
“Tuende katika Swala ya Iddi tukiwa na nyoyo safi, tukimshukuru Mwenyezi Mungu na kuliombea taifa letu,” alihitimisha.
Ends.


0 Comments