TAKUKURU ARUSHA YARIDHISHWA NA MATUMIZI YA BILIONI 2.5 MIRADI YA MAENDELEO
Yasema mapendekezo 7 yatekelezwa kwa asilimia 100, yachochea ubora na thamani ya fedha
Na Joseph Ngilisho | Arusha
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imeridhishwa na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.5, iliyotekelezwa katika sekta za afya, elimu na miundombinu, hatua inayotajwa kuimarisha uwajibikaji na thamani ya fedha za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 18, 2026, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngajilo alisema kuwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025, taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji wa kina wa matumizi ya fedha hizo katika miradi mitano ya maendeleo mkoani humo.
Alisema ufuatiliaji huo haukuishia tu katika kubaini matumizi sahihi ya fedha, bali pia ulichochea kukamilika kwa miradi hiyo kwa kuzingatia ubora unaolingana na thamani ya fedha pamoja na uhalisia wa bajeti zilizopangwa.
“Mkoa ulitoa mapendekezo saba yaliyolenga kuboresha usimamizi wa miradi na kuondoa mianya ya rushwa, na yote yametekelezwa kwa asilimia 100. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa miradi hiyo kwa viwango vinavyokidhi thamani ya fedha za umma,” alifafanua Ngajilo.
Kwa mujibu wa TAKUKURU, utekelezaji huo umeonesha matokeo chanya ya usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo, hususan katika kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa bila upotevu au ubadhirifu.
Uchunguzi na mashtaka yaimarika
Katika hatua nyingine, TAKUKURU ilibainisha kuwa utekelezaji wa maazimio 23 yaliyotokana na uchambuzi wa mifumo katika sekta za afya, ardhi na utawala kupitia Dawati la Kuzuia Rushwa umefikia asilimia 100, hatua inayotajwa kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ndani ya taasisi za umma.
Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya malalamiko 66 yalipokelewa, ambapo asilimia 68 yalihusu tuhuma za rushwa. Kutokana na uchunguzi uliofanyika, kesi 15 zilifunguliwa mahakamani, huku kesi mbili zikiwa tayari zimeshapata ushindi.
Mkakati mpya kuimarisha ufuatiliaji
Ngajilo alieleza kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, TAKUKURU imejipanga kuimarisha zaidi ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kudhibiti mianya ya rushwa katika matumizi ya fedha za umma.
Alisisitiza kuwa ufuatiliaji huo utafanyika katika ngazi zote kuanzia mkoa, wilaya, kata hadi mitaa na vijiji, kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa miradi unazingatia vigezo, ubora na uwazi unaohitajika.
“TAKUKURU itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na hatimaye kufikia azma ya utawala bora kwa wananchi,” alibainisha.
Wito kwa wananchi
Katika hatua ya kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, TAKUKURU Mkoa wa Arusha imewahakikishia wananchi ushirikiano wa dhati na kuwataka kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ili kusaidia juhudi za serikali katika kulinda rasilimali za umma.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inaleta tija kwa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
Ends..


0 Comments