VIONGOZI watatu wa Umoja wa Bodaboda Jiji la Arusha (UBOJA) akiwemo Mwenyekiti wao Costantine Okelo, Katibu Hakimu Msemo, na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Hemedi maarufu kama Osama, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa zaidi ya wiki moja wakikabiliwa na tuhuma za kula fedha za kampeni zinazokadiriwa kufikia shilingi milioni 30.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa viongozi hao walipokea kopon za mafuta kutoka chama kimoja cha siasa jijini Arusha, kwa lengo la kuwawezesha madereva wa bodaboda na bajaji wapatao 200 kumkaribisha kiongozi wa chama hicho aliyekuwa akifanya ziara ya kisiasa mkoani humo. Kila dereva alitarajiwa kuwekewa mafuta ya thamani ya lita nne kupitia uratibu wa viongozi wao.
Hata hivyo, badala ya fedha hizo kufika kwa walengwa, imeelezwa kuwa viongozi hao waligawa kopon chache kwa baadhi ya madereva, huku kopon nyingine wakiziuza na kuchukua fedha taslimu, kinyume na makubaliano yaliyowekwa kati ya chama hicho na kituo kimoja maarufu cha mafuta jijini Arusha.
Vurugu Zazuka Kituo cha Mafuta
Mwanzoni mwa wiki hii, zaidi ya madereva 100 wa bodaboda na bajaji walijikusanya na kuvamia kituo hicho cha mafuta wakishinikiza kupewa mafuta waliyokuwa wameahidiwa. Tukio hilo lilisababisha taharuki kubwa kwa zaidi ya saa sita, baada ya mmiliki wa kituo hicho kukataa kutoa mafuta akidai hajalipwa na chama husika.
Baada ya majadiliano marefu kati ya viongozi wa chama na uongozi wa kituo hicho, makubaliano mapya yalifikiwa majira ya saa nane mchana, na madereva wakaanza kupewa mafuta — hali iliyorejesha utulivu, japokuwa wengine walilalamika kutopata haki yao kikamilifu.
“Tumechoka Kutumiwa na Wanasiasa” — Madereva
Baadhi ya madereva wa bodaboda waliozungumza na Arushadigital walisema wanahisi kutumiwa kisiasa kila mara uchaguzi au mikutano mikubwa inapokaribia, lakini baada ya hapo husahauliwa kabisa.
“Kila kipindi cha kampeni tunaitwa, tunaahidiwa mafuta, fulana na posho, lakini mwisho wa siku tunapotezwa. Tumechoka kuwa ngazi ya wanasiasa,” alisema Juma Mollel, dereva wa bodaboda eneo la Unga Ltd.
Dereva mwingine, Nasri Rashid, alisema:
“Tunafanya kazi ngumu, lakini kila mara tunadanganywa. Wanasiasa wanatutumia kwa manufaa yao halafu wakipata wanatoweka. Huu ni udhalilishaji, na tunataka serikali ichukue hatua kwa wote waliohusika.”
Polisi Wathibitisha Kuwashikilia
M
Polisi mkoani Arusha wamethibitisha kuwa viongozi hao wa UBOJA wako mikononi mwao kwa mahojiano zaidi, huku taarifa zikidai kuwa mmoja kati ya watuhumiwa wanne ametoweka na anatafutwa.
Chanzo kutoka ndani ya Jeshi la Polisi kimesema kuwa upelelezi umekamilika kwa kiasi kikubwa, na kuna uwezekano mkubwa watuhumiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu, Oktoba 13, 2025, kujibu tuhuma za udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Hadi tunapokwenda mitamboni, jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo, ili kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu tukio hilo hazikufanikiwa, kwani simu yake ilikuwa haipatikani.
Ends..




0 Comments