Na Joseph Ngilisho, Arusha
ZAIDI ya wafanyakazi 600 wa Hospitali ya Rufaa ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wapo katika hali ngumu ya maisha baada ya kudaiwa kutolipwa mishahara yao kwa zaidi ya miezi 15, hali ambayo imesababisha huduma nyingi hospitalini hapo kudorora kwa kiwango cha kutia wasiwasi.
Hospitali hiyo, ambayo kwa miaka mingi imekuwa tegemeo kwa wananchi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na sehemu za Kenya, sasa inatajwa kuwa katika hali ngumu ya kifedha huku baadhi ya wafanyakazi wakishindwa hata kufika kazini kutokana na ukata.
Jana (Jumatatu) oktoba 27,2025, zaidi ya wafanyakazi 100 wakiwemo wauguzi, madaktari wasaidizi, wahudumu wa usafi na madereva walikusanyika eneo la mapokezi ya hospitali hiyo kwa lengo la kufanya mgomo baridi, wakipinga kucheleweshwa mishahara yao kwa muda mrefu.
Baada ya muda, uongozi wa hospitali ulidaiwa kutoa vitisho vya kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi, jambo lililosababisha baadhi ya wafanyakazi kuingiwa na hofu na kurejea kazini huku wengine wakiendelea na mgomo kimya kimya.
“Tunateseka, lakini tunaogopa kusema”Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa hofu ya kufukuzwa kazi, walisema wamefika hatua ya kuomba msaada wa chakula na makazi kutoka kwa ndugu na marafiki kutokana na hali ngumu ya maisha.
> “Tunaishi kwa neema tu. Wengine tumefukuzwa kwenye nyumba za kupanga, watoto wameshindwa kwenda shule, na hata chakula ni tatizo. Tunafanya kazi kwa moyo lakini bila matumaini,” alisema mmoja wa wauguzi wa wodi ya wazazi.
Madaktari wachache waliobaki wamekuwa wakifanya kazi kwa zamu ndefu bila mapumziko, jambo linaloongeza uwezekano wa makosa ya kitabibu.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa ALMC, Dkt. Godwil Kivuyo, alikanusha kuwepo kwa mgomo au malalamiko makubwa, akisema:
> “Sifahamu kuhusu mgomo wala madai hayo. Hakuna mfanyakazi aliyefukuzwa kazi kwa sababu ya kudai mshahara. Masuala ya malipo ni ya kiutawala, hivyo siwezi kuyazungumzia kwa undani.”
Kwa upande wake, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Solomoni Sambweti, alikiri kuwapo kwa changamoto ya mishahara, lakini akasema tatizo hilo limesababishwa na kushuka kwa mapato ya hospitali kutokana na gharama kubwa za uendeshaji na wingi wa wagonjwa wasiolipa.
> “Ni kweli wafanyakazi wanadai mishahara, lakini tumeanza mchakato wa ndani kuhakikisha malimbikizo hayo yanapungua. Hakuna anayefukuzwa kwa sababu ya kudai haki yake,” alisema Sambweti.
Tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya 40% ya wahudumu wa afya huanza kutafuta kazi nyingine au kuondoka nchini wanapocheleweshwa mishahara kwa zaidi ya miezi sita. Hali kama hii ikiendelea ALMC, kuna hatari hospitali ikapoteza wataalamu muhimu.
Kwa kuwa ALMC inamilikiwa na kanisa, ucheleweshaji wa mishahara kwa miezi 15 unahatarisha uaminifu wa jamii kwa taasisi za dini zinazomiliki huduma za kijamii.
Wadau wa afya jijini Arusha wameiomba Serikali, Kanisa la KKKT, na mashirika ya kimataifa ya afya kama ELCT Health Board na Lutheran World Federation kuingilia kati ili kuokoa taasisi hiyo muhimu isidhoofike zaidi.
> “ALMC ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini. Ikiendelea hivi, wananchi watakosa huduma muhimu za afya. Serikali inapaswa kuingilia kati haraka,” alisema mmoja wa wadau wa afya mkoani Arusha.
Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center, iliyoanzishwa mwaka 2000, imekuwa moja ya vituo vinavyotoa huduma za rufaa na upasuaji mkubwa kwa zaidi ya wagonjwa 90,000 kila mwaka, lakini sasa iko katika changamoto kubwa ya kifedha na kiutawala, ikihitaji hatua za haraka ili kurejesha ufanisi wake.
-Ends..

0 Comments