DC ARUSHA AWAHAKIKISHIA USALAMA WANANCHI SIKU YA UCHAGUZI ADAI MAANDAMANO YATAKAYOKUWEPO NIYAKUPIGA KURA TU

 

MKUU WA WILAYA ARUSHA AHAKIKISHA USALAMA KATIKA UCHAGUZI OKTOBA 29

Na ArushaDigital – Arusha


MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amewatoa hofu wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwahakikishia usalama wa kutosha katika zoezi la kupiga kura litakalofanyika Oktoba 29, 2025, huku akiwataka kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo muhimu wa Rais, Wabunge na Madiwani.


Akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi yake jijini Arusha, Mkude alisema taarifa zinazoenezwa mitandaoni kuhusu uwepo wa maandamano au uvunjifu wa amani hazina ukweli wowote, akisisitiza kuwa maandamano pekee yatakayokuwepo ni “maandamano ya kwenda kupiga kura.”

> “Tumejipanga vizuri kuhakikisha kila kitu kinaenda kwa amani. Hali ya usalama katika wilaya yetu ni ya kuridhisha kabisa. Hakutakuwa na vurugu wala maandamano kama inavyodaiwa mitandaoni. Wananchi waende wakapige kura kwa amani,” alisema Mkude.


Alibainisha kuwa wilaya ya Arusha ina jumla ya wapiga kura 435,119 ambao watapiga kura katika vituo 1,051 vilivyogawanyika katika mitaa 154.

Aidha, alisema jumla ya vyama 17 vya siasa vilichukua fomu za kushiriki uchaguzi huo, lakini chama kimoja hakikurudisha fomu, hivyo vyama 16 ndivyo vitakavyoshiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.

Mkude aliongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mgombea Urais kupitia CCM, ametangaza siku ya Jumatano, Oktoba 29, kuwa ni siku ya mapumziko ili wananchi wote wapate nafasi ya kushiriki uchaguzi bila vikwazo.

> “Kipindi cha kampeni kimekuwa cha amani. Vyama vyote vilipewa nafasi sawa ya kujinadi na kulindwa na vyombo vya usalama. Sasa kinachotakiwa ni wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, kwa sababu siku hiyo hakuna kazi,” alisisitiza Mkude.


Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Daudi Mrema, alisema anapongeza hatua ya serikali kuhakikisha usalama wakati wa uchaguzi, lakini akasisitiza umuhimu wa usalama kuendelea hadi baada ya matokeo kutangazwa.

> “Ni jambo jema kuona serikali inatoa uhakika wa amani. Tunachotaka kuona ni haki ikitendeka, wananchi wakipiga kura bila hofu, na matokeo yakiheshimiwa. Hapo ndipo demokrasia inaimarika,” alisema Mrema.


Nao wananchi wa jiji la Arusha wamempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kauli hiyo, wakisema imetuliza hofu iliyokuwa imeanza kuenea mitaani.

Bi. Amina Mollel, mkazi wa Ngarenaro, alisema wananchi wengi walikuwa na wasiwasi kutokana na taarifa zilizokuwa zikisambaa mtandaoni.

> “Kauli hii imetupa amani. Mimi binafsi nitajitokeza kupiga kura mapema, maana sasa naamini hakutakuwa na vurugu. Tunataka kuona amani inatawala kama alivyoahidi Mkuu wa Wilaya,” alisema Mollel.


Mkude alimalizia kwa kusema kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vimekamilika na vitaanza kusambazwa katika vituo vyote vya kupigia kura haraka iwezekanavyo, ili kuhakikisha zoezi linaanza kwa wakati na linafanyika kwa utulivu.

Ends .

Post a Comment

0 Comments