MGOMBEA UBUNGE MONDULI JOSEPH ISAAK AFUNGA KAMPENI KWA KISHINDO MTO WA MBU
Na Joseph Ngilisho-Monduli
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Monduli kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joseph Isaak, amefunga kampeni zake kwa kishindo katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika kata ya Mto wa Mbu, akiahidi kusimamia kwa ufanisi miradi yote aliyoahidi kwa wananchi pamoja na miradi mikubwa iliyoahidiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wilayani humo.
Mkutano huo uliofurika mamia ya wananchi, wakiwemo wafugaji, vijana na kina mama, ulihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Frederick Sumaye, ambaye alihitimisha rasmi kampeni za chama hicho katika jimbo la Monduli.
Akihutubia umati wa wananchi waliokuwa wamefurika katika uwanja wa Mto wa Mbu, Joseph Isaak — anayefahamika zaidi kwa jina la “Kadogoo” — aliwahakikishia wananchi kuwa atakuwa kiungo muhimu kati yao na serikali ya Rais Samia katika kuhakikisha ahadi zote zinatimia kwa wakati.
> “Nawaahidi kuwa nitakuwa mbunge wa vitendo, nitakayesimamia utekelezaji wa miradi yote tuliyoahidi pamoja na miradi mikubwa ya Rais Samia hapa Monduli. Sitakaa ofisini, nitakuwa na ninyi vijijini kuhakikisha maendeleo tunayoyaahidi yanakuwa halisi,” alisema Isaak huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Miongoni mwa ahadi zake kwa wakazi wa kata ya Mto wa Mbu ni,Kutatua mgogoro kati ya wananchi na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA);
Kushughulikia korongo na mitaro inayoathiri makazi na mashamba,Kuboresha soko la Mto wa Mbu na kuwezesha mikopo kwa wanawake na makundi maalum;
Kuboresha miundombinu ya barabara, na Kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinakuwa na zahanati ya kutoa huduma za afya za uhakika.
Isaak pia aliahidi kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa iliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan wilayani Monduli, ikiwemo:
Ujenzi wa mabweni 90 kwa shule za msingi na sekondari,Ujenzi wa nyumba 300 za walimu,Ofisi 54 za vijiji na 8 za kata,Shule mpya 5 za msingi na 5 za sekondari.
Ujenzi wa matundu 15,000 ya vyoo katika shule za msingi na sekondari,Ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilometa 54 kwa kiwango cha lami,Madaraja 8 mapya, na Ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Monduli.
> “Miradi hii ni alama ya uongozi wa Rais Samia na tumeona kazi zake zikigusa kila kona ya nchi. Nikiwa mbunge wenu, nitahakikisha Monduli haiachwi nyuma,” aliongeza Isaak.
Akifunga rasmi kampeni hizo, Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Frederick Sumaye, aliwataka wananchi wa Monduli kujitokeza kwa wingi kesho kupiga kura kwa amani, wakimchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Joseph Isaak (Kadogoo), na madiwani wote wa CCM.
> “CCM ndiyo chama pekee kinachotekeleza, si cha maneno bali cha vitendo. Tumwongezee nguvu Rais Samia kwa kumpa wabunge na madiwani wa chama chake ili aendelee kutuletea maendeleo,” alisema Sumaye huku akipigiwa makofi na wananchi.
Miongoni mwa wageni waliohudhuria mkutano huo mkubwa wa kufunga kampeni ni mfanyabiashara maarufu wa Mto wa Mbu na Arusha, Deepyen Barmeda, ambaye aliahidi kushirikiana na serikali na wabunge wa CCM katika kuendeleza sekta za biashara, utalii na kilimo wilayani Monduli.
Kufungwa kwa kampeni hizo kunatizamwa kama mwisho wenye hamasa kubwa zaidi katika historia ya kisiasa ya Monduli, ambapo wananchi wameonyesha imani kubwa kwa mgombea huyo kijana, wakisema wanataka mbunge wa vitendo anayeishi na wananchi.
> “Tunamwamini Kadogoo kwa sababu ameishi nasi, anajua shida zetu na haogopi kusema ukweli. Huyu ni kiongozi wa watu,” alisema mzee Lembris Nanyori, mkazi wa Mto wa Mbu.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika kesho, Oktoba 29, 2025, ambapo wananchi wa Monduli wataamua nani ataendelea kuwatumikia kwa kipindi kijacho cha miaka mitano
-ends











0 Comments