POLISI AUAWA KWA KUPIGWA MSHALE NJE YA LANGO LA IKULU
Na Arushadigital — Nairobi
Tukio la kusikitisha limetokea jijini Nairobi, Kenya, baada ya askari polisi aliyekuwa kazini katika lango la Ikulu kuuawa kwa kupigwa mshale na mtu anayedaiwa kuwa na matatizo ya akili.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Kenya, polisi huyo aliyetambuliwa kwa jina Ramadhan Mattanka, alipigwa mshale kifuani na mwanaume mmoja aliyekuwa amebeba upinde na mishale, tukio lililotokea muda mfupi baada ya afisa huyo kumtaka mtuhumiwa huyo kuondoka eneo hilo.
Mashuhuda walisema kuwa, baada ya mashambulizi hayo, polisi wenzake walikimbia kumsaidia Mattanka na kumkimbiza katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), ambako madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake, lakini alifariki dunia akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Mtuhumiwa huyo, anayefahamika kwa jina Kithuka Kimunyi, alikamatwa muda mfupi baadaye na anashikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano.
Msemaji wa Polisi nchini Kenya alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa kina umeanzishwa ili kubaini mazingira ya tukio hilo na nia halisi ya mtuhumiwa kufanya shambulio hilo hatari.
“Ni tukio la kusikitisha sana. Tumempoteza askari shupavu ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake ya ulinzi wa taifa kwa uadilifu mkubwa,” alisema msemaji huyo.
Kwa sasa eneo la tukio limewekwa chini ya ulinzi mkali huku mamlaka za usalama zikiendelea na uchunguzi ili kuhakikisha usalama unaimarishwa katika maeneo yote yanayozunguka Ikulu.
Wakati tukio hilo likiripotiwa nchini Kenya ,hapa nchini tukio linalomhusu askari polisi jijini Arusha ,Omari Mnandi aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwa na kusababisha kifo chake ,hata hivyo matukio hayo hayana mahusiano.
#Arushadigital inakupa habari mpya na moto moto endelea kutuamini#
Ends..

0 Comments