MWENYEKITI WA KIJIJI CHA KISERIANI MATATANI AHUSISHWA NA UUZWAJI WA ENEO LA HIFADHI KWA MWEKEZAJI
Na Joseph Ngilisho— Arumeru
Mvutano mkali umeibuka katika Kijiji cha Kiseriani, wilayani Arumeru, mkoani Arusha, baada ya wananchi kumtuhumu mwenyekiti wa kijiji hicho, Maliaki Loisulie Mollel, kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka, kukosa uwazi katika miradi ya maendeleo na kupokea fedha kutoka kwa mwekezaji bila ridhaa ya wananchi.
Taarifa kutoka kwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho zinasema kuwa mwenyekiti huyo alishawahi kuwekwa kizuizini kwa siku kadhaa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatia malalamiko ya wananchi wanaodai alipokea kiasi cha fedha kutoka kwa mwekezaji aliyenunua sehemu ya ardhi ya kijiji katika eneo la Mlima wa Kiseriani,jambo ambalo amelikanusha vikali.
Inadaiwa kuwa mwekezaji huyo aliahidi kujenga ofisi ya kijiji kama sehemu ya makubaliano ya uwekezaji huyo, lakini hadi sasa hakuna dalili zozote za utekelezaji wa ahadi hiyo, hali iliyowafanya wananchi kuhoji ni nani ananufaika na mpango huo.
“Tumekuwa tukiahidiwa kila mara kwamba mwekezaji atajenga ofisi ya kijiji,atakarabati barabara zetu kwa kiwango cha changarawe, lakini muda unapita hatuoni lolote. Hatujui utekelezaji huo, wala nani anasimamia hilo,” alisema mmoja wa wananchi (jina limehifadhiwa).
MAELEZO YA MWENYEKITI MOLLEL
Akizungumza na Arushadigital, mwenyekiti wa kijiji hicho, Maliaki Loisulie Mollel, amekanusha tuhuma hizo akisema suala hilo limepotoshwa na baadhi ya watu wasiokitakia , mema kijiji hicho ,wakiwa na maslahi yao binafsi.
Mollel alieleza kuwa mwaka 2024 kulitokea mwekezaji aliyeonesha nia ya kuwekeza katika eneo la kijiji, na wakati huo kulikuwa na uongozi mwingine wa kijiji uliokuwa madarakani ambao, kwa kushirikiana na wananchi wenye maeneo na serikali ya kijiji, waliingia makubaliano rasmi kwa kusaini nyaraka za mauziano ya eneo lenye ukubwa wa ekari 70, likihusisha vijiji viwili vilivyopo katika eneo la mlima huo.
“Kulikuwa na makubaliano halali kabisa. Uongozi uliokuwepo kabla yetu, wananchi wenye ardhi na mwekezaji walitia saini nyaraka rasmi na kukubaliana kuwa fedha za mauzo zitalipwa ndani ya muda fulani,” alisema Mollel.
Amefafanua kuwa baada ya kuingia madarakani mwaka huu, alikutana na mwekezaji huyo na kufanya mazungumzo mapya yaliyolenga kuhakikisha kijiji kinanufaika na uwekezaji huo.
“Tulikubaliana kuwa katika mradi wake, mwekezaji atatekeleza baadhi ya miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa ofisi ya kijiji na ujenzi wa barabara katika kiwango cha changarawe ili kuimarisha maendeleo ya eneo letu,” aliongeza.
Mwenyekiti huyo alikiri kuwa alishikiliwa na TAKUKURU kwa mahojiano, lakini akabainisha kuwa hatua hiyo ilihusiana na jitihada zake za kutaka wananchi waliouzia ardhi walipwe stahiki zao.
“Ni kweli nilishikiliwa na TAKUKURU, lakini si kwa makosa ya rushwa kama inavyodaiwa. Nilikuwa napigania haki ya wananchi waliouzia maeneo yao kwa mwekezaji. Nilipambana kumtafuta mwekezaji huyo na nilipompata alinieleza kuwa ameshindwa kuwalipa wananchi kwa wakati kwa sababu mikataba yake ilikuwa imechukuliwa na TAKUKURU kwa uchunguzi,” alisema Mollel.
Alisema baada ya mahojiano hayo, TAKUKURU walimwachia huru ila uchunguzi wa suala hilo bado unaendelea kwa madai kwamba maeneo hayo yameuzwa kinyume cha sheria kwa kuwa maeneo hayo yaliuzwa kinyume ni maeneo ya hifadhi .Pia alisema kuhusu nyaraka za mwekezaji na mwananchi bado zipo nikononi mwa takukuru kwa sababu ya uchunguzi.
Mollel pia alisisitiza kutohusika na fedha zozote za makubalino na mwekezaji akidai hakuna hata senti moja aliyochukua ila anachoamini kuna wananchi hawapendi maendeleo anayofanya katika kijiji hicho ndio wanaopandikiza chuki.
Kuhusu ukarabati wa Shule ya Msingi Kiseriani, Mollel alikanusha madai ya ubadhirifu, akieleza kuwa mradi huo unaendelea vizuri kwa kufuata viwango na taratibu za serikali.
“Ukarabati unaendelea vizuri na kwa ubora unaotakiwa. Serikali ilitoa fedha, na tumehakikisha matumizi yanafuata kanuni zote. Wananchi wapewe taarifa sahihi na si maneno ya mitaani,” alisisitiza mwenyekiti huyo.
MALALAMIKO YA WANANCHI YANAENDELEA
Hata hivyo, licha ya maelezo hayo, baadhi ya wananchi bado wanadai hawajaridhishwa na uwazi wa mwenyekiti katika utoaji wa taarifa za miradi na mikataba ya uwekezaji.
Wanaitaka serikali ya wilaya na taasisi husika kufanya uchunguzi wa kina ili kuweka ukweli hadharani na kurejesha imani ya wananchi kwa uongozi wa kijiji hicho.
Ends...

0 Comments