Mkude Aipongeza Taasisi ya Nasimama na Mama kwa Kuitangaza Serikali
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ameisifu Taasisi ya Nasimama na Mama Tanzania (TNMT) kwa mchango wake mkubwa katika kusimama mstari wa mbele kueneza taarifa sahihi juu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa taasisi hiyo uliofanyika kwenye viwanja vya Jengo la Azimio la Arusha, Mkude alisema uamuzi wa TNMT ni wa kupongezwa kwa kuwa unaondoa upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wanaodai kwamba serikali haijafanya chochote.
“Ni wakati wa vikundi na taasisi zingine kuiga mfano huu, kwa sababu kuna miradi mingi mikubwa na midogo imefanywa na serikali. Sasa ni lazima jamii ipate taarifa sahihi ili ijue serikali yao inafanya kazi kubwa kwa maslahi ya Taifa,” alisema Mkude.
Aidha, alisifu hatua ya taasisi hiyo kutenga Shilingi milioni 150 kwa ajili ya mikopo kwa vijana na wanawake katika kata 15 za Jiji la Arusha. Mikopo hiyo imelenga kuwasaidia kwenye miradi ya ujasiriamali ili kupunguza changamoto ya ajira na kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Mkude alisisitiza kuwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni mwanzo mzuri na akawataka viongozi wake kujitoa kwa dhati ili kulinda heshima na uaminifu wa TNMT mbele ya jamii na serikali.
Taasisi Kujikita Kukuza Uchumi na Kutoa Elimu
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TNMT Kanda ya Kaskazini, Monica Suleiman, alisema taasisi hiyo inafanya kazi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara. Lengo lake kuu ni kuieleza jamii kwa kina miradi na kazi zinazofanywa na serikali, sambamba na kutoa fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake.
Alifafanua kuwa kwa kuanzia, kila kikundi katika kata 15 za Jiji la Arusha kitapewa Shilingi milioni 10. Kila kikundi kitahusisha vijana au wanawake wasiozidi kumi, watakaotambulika rasmi na viongozi wa serikali ngazi ya kata.
“TNMT imejipanga kuwa daraja la kuwasaidia vijana na wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba. Tutawawezesha kuanzisha miradi kama ya ufugaji na kilimo badala ya kutegemea ajira za serikali ambazo ni chache,” alisema Monica.
Aliongeza kuwa kabla ya vikundi hivyo kupatiwa fedha, watapatiwa elimu ya ujasiriamali ili kuhakikisha miradi inayoanzishwa inakuwa endelevu.
Malengo ya Kitaifa
Naye Muasisi wa TNMT, Ibrahimu Mwakabwanga, alisema taasisi hiyo kwa sasa ipo katika mikoa zaidi ya mitano, huku malengo yakiwa ni kufanikisha upanuzi hadi kufika mikoa yote nchini.
“Tunataka kila sehemu nchini kuwe na mwamko wa kuzungumzia maendeleo ya serikali kwa uwazi na uhalisia, sambamba na kuwasaidia wananchi kupitia mikopo na elimu ya kiuchumi,” alisema Mwakabwanga.
Ends...



0 Comments