Maelfu Wamlaki Rais Samia Arusha, Makonda Amnadi na Kumshukuru
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
Maelfu ya wakazi wa Arusha Mjini leo (2 Oktoba 2025) wamefurika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid kushuhudia uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paul Makonda, alisimama jukwaani kumwaga sifa na kumtambulisha rasmi mgombea urais kupitia CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Makonda aliwahutubia wananchi kwa msisitizo mkubwa leo oktoba 2,2025 akieleza namna Dkt. Samia alivyoacha alama isiyofutika katika mkoa wa Arusha kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Uwanja wa Ndege wa Arusha: Mlango Mpya wa Biashara na Utalii
Akigusia moja kwa moja miradi hiyo, Makonda alieleza jinsi upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Arusha ulivyoleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii. Kwa mara ya kwanza, ndege kutoka nje ya nchi zinatua moja kwa moja jijini Arusha bila ya kupitia viwanja vingine kupata vibali.
“Hii ni hatua kubwa ya kufungua milango ya utalii na biashara. Wafanyabiashara sasa hawapotezi muda wala fedha nyingi, na watalii wanaingia moja kwa moja kuiona Tanzania,” alisema Makonda huku akishangiliwa na umati.
Miradi Mikubwa Inayoinua Jiji
Makonda hakusita kuorodhesha mafanikio mengine. Alibainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 64 zimetumika kutekeleza miradi iliyokuwa imekwama kwa miaka mingi, ikiwemo:
- Ujenzi wa Stendi Kuu ya Kisasa ya Mkoa wa Arusha,
- Soko kubwa na la kisasa katikati ya jiji,
- Mradi wa umeme wa REA unaowawezesha wananchi kuunganishiwa huduma kwa Shilingi 27,000 pekee.
Kwa mujibu wake, mafanikio hayo ni ushahidi halisi wa uongozi imara wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia.
Shukrani na Ujumbe wa Heshima
Akitumia nafasi hiyo, Makonda alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumuamini na kumpa nafasi mbalimbali za uongozi.
“Kipekee nakushukuru Mama Samia kwa nyakati zote kuniamini na kunipa heshima kubwa kama kiongozi wa vijana, mkuu wa mkoa wa Arusha na sasa kupitia kura za maoni kunirudisha tena kugombea ubunge wa Jimbo hili. Hii ni heshima kubwa kwangu na kwa wananchi wa Arusha,” alisema Makonda.
Kwa sauti yenye hisia, Makonda alimalizia kwa maneno yenye kugusa umati:
“Mama Samia wewe ni mama mwema sana. Hujawahi kuacha vijana nyuma. Mungu wa mbinguni akulinde na akupe nguvu kuendelea kuongoza taifa hili.”
Ends..
0 Comments