LAIGWANANI WAAHIRISHA SHEREHE ZA TOHARA KUPISHA UCHAGUZI ,WAHAMASISHA VIJANA KUPIGA KURA

KIONGOZI MKUU WA KIMILA WA JAMII YA KIMASAI AHIRISHA TOHARA KUWAWEZESHA VIJANA KUPIGA KURA

Na Joseph Ngilisho – Arusha


Kiongozi Mkuu wa Kimila wa Jamii ya Kimasai nchini (Laigwanani), Isack Ole Kisongo Meijo, ametangaza kusogezwa mbele kwa zoezi la tohara la vijana wa jamii hiyo lililokuwa lifanyike kuanzia Oktoba 21 hadi 30, mwaka huu, ili kutoa fursa kwa zaidi ya vijana 2,000 waliotarajiwa kushiriki kwenye tohara hiyo kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Ole Kisongo alitoa kauli hiyo leo, Oktoba 17, 2025, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, wakati wa kikao cha Baraza la Maigwanani Mkoa wa Arusha, akisisitiza kuwa jamii ya Kimasai imeamua kwa pamoja kuhakikisha inashiriki kwa wingi katika uchaguzi huo huku ikidumisha amani.

> “Hiyo siku ni takatifu katika Taifa la Tanzania. Tumeambiana kuwa hatutaki kushika mkia. Tunataka kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika vijiji vyetu. Ukitahiri vijana 1,000 leo, utapunguza kura kwani mgonjwa hatoweza kwenda kupiga kura. Tunataka wote tushiriki ipasavyo,”alisema Ole Kisongo.



Amesema uamuzi huo ni sehemu ya dhamira ya jamii ya Kimasai kuhakikisha vijana wake wanatumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kushiriki katika maamuzi ya maendeleo ya Taifa, huku akiihakikishia serikali kuwa jamii hiyo itaendelea kuwa nguzo ya amani katika kipindi chote cha uchaguzi.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, aliipongeza jamii ya Kimasai kwa uamuzi huo wa kizalendo na kueleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya uelewa mkubwa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu.

> “Nawapongeza sana kwa kuonesha uzalendo na utambuzi wa umuhimu wa amani. Serikali ya awamu ya sita inatambua na kuthamini juhudi zenu. Endeleeni kuwa mabalozi wazuri wa amani na hamasa ya kujitokeza kupiga kura,”alisema Makalla.


Aliongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha Mkoa wa Arusha unabaki kuwa salama kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu, huku akiwataka wananchi kurejea majumbani mara baada ya kupiga kura na kuziachia mamlaka husika kusimamia mchakato wa ulinzi wa kura.

> “Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu. Wananchi wanapaswa kuendelea kudumisha mshikamano na kuilinda nchi yetu,”alisisitiza CPA Makalla.





Ends..

Post a Comment

0 Comments