CCM Yaonywa na NEC kwa Ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi Kigoma
Na Arushadigital – Kigoma
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kupitia Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini, David Rwazo, imetoa onyo kali kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kigoma, baada ya kubainika vitendo kadhaa vinavyokiuka Kanuni za Maadili ya Uchaguzi vinavyofanywa na baadhi ya wanachama na wagombea wa chama hicho katika kipindi cha kampeni.
Katika barua rasmi iliyotumwa Oktoba 16, 2025 kwa Katibu wa CCM mkoa wa Kigoma, ambayo Jambo TV imeiona, Rwazo alisema Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Jimbo hilo ilikutana Oktoba 15, 2025 na kujadili mwenendo wa kampeni. Kikao hicho kilibaini vitendo vya ukiukwaji wa maadili vinavyohusishwa na chama hicho katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Miongoni mwa makosa yaliyotajwa ni pamoja na kung’oa na kuchana mabango ya Chama cha ACT Wazalendo, kufanya mikutano nje ya ratiba, kutumia lugha za matusi na kejeli dhidi ya mgombea wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) katika kata ya Rubuga, pamoja na kuingilia misafara ya vyama vingine vya siasa.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya wanachama wa CCM wamekuwa wakifunika mabango ya ACT Wazalendo katika maeneo ya wazi, hususan eneo la Roundabout Mwanga, jambo lililotajwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili na ushindani wa haki.
Katika barua hiyo, Rwazo pia amelaani kitendo cha mgombea udiwani wa CCM katika kata ya Katubuka, Daniel Rumenvela, kwa kumtolea lugha za matusi Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa ngazi ya kata, akisisitiza kuwa kitendo hicho hakikubaliki na hakipaswi kujirudia tena.
> “Kwa mujibu wa Kanuni ya 4.1(g) ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ina wajibu wa kukemea vitendo vyenye uwezekano wa kuharibu mchakato wa uchaguzi vinavyoweza kufanywa na viongozi wa vyama, wagombea, wanachama, serikali na watendaji wake,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Rwazo aliongeza kuwa, endapo CCM au wagombea wake wataendelea na vitendo hivyo, Tume haitasita kusitisha mikutano yao ya kampeni iliyosalia katika jimbo hilo, ili kulinda heshima na utulivu wa uchaguzi.
Kadhalika, amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kufuatilia kwa karibu shughuli za kampeni katika maeneo yote ya Kigoma na kuchukua hatua za kisheria pale panapothibitika ukiukwaji wa kanuni za maadili.
Amesisitiza kuwa wadau wote wa uchaguzi, wakiwemo vyama vya siasa, wagombea, na wafuasi wao, wanapaswa kuhakikisha kampeni zinafanyika kwa amani, heshima, na kwa kuzingatia sheria.
Kauli za Wadau wa Kisiasa
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoa wa Kigoma, Ramadhan Mselem, ameupongeza uamuzi wa NEC kwa kuchukua hatua ya kukemea vitendo vya ukiukwaji wa maadili, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda uwanja sawa wa ushindani.
> “Tumekuwa tukilalamika mara kwa mara kuhusu mabango yetu kung’olewa na kufunikwa, pamoja na wafuasi wetu kuzuiwa kufanya kampeni katika baadhi ya maeneo. Tunashukuru kwamba NEC imechukua hatua kwa haki. Tunataka uchaguzi wa amani na usawa kwa vyama vyote,” alisema Mselem.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kampeni wa CHAUMMA kata ya Rubuga, Amina Katembo, alilaani kitendo cha baadhi ya wanasiasa kutumia lugha za kejeli na matusi kwenye majukwaa ya kampeni, akisema vitendo hivyo vinaweza kuchochea chuki na kuvuruga amani.
> “Uchaguzi ni ushindani wa hoja, si wa matusi wala vitisho. Tunatoa wito kwa wagombea wote kuzingatia maadili na kuheshimiana. Tunatarajia Tume itaendelea kuwa makini katika kusimamia haki,” alisema Katembo.
Naye Katibu wa CCM mkoa wa Kigoma, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema chama hicho kimepokea barua hiyo na kipo tayari kushirikiana na Tume kuhakikisha kampeni zinabaki ndani ya mipaka ya maadili.
> “Tunachukulia maelekezo haya kwa uzito. Kama kulikuwa na makosa, tutayafanyia kazi. CCM inaamini katika amani, umoja, na utii wa sheria,” alisema kiongozi huyo.
Barua hiyo kutoka NEC imetolewa ikiwa zimesalia takribani wiki mbili kabla ya kufungwa rasmi kwa kampeni za uchaguzi ambapo wadau wengi wameitaka Tume kuendelea kuwa makini kuhakikisha kanuni za maadili zinazingatiwa na vyama vyote bila upendeleo.
Chanzo Jambo Tv
Ends..

0 Comments