WANANCHI OLASITI NI KILIO CHA KUKOSA MAJI WAKESHA WAKICHOTA MAJI MTONI NDOA ZAO HATARINI,WAZIRI AWEZO AIJIA JUU AUWSA

Na Joseph Ngilisho, Arusha

 

Zaidi ya wakazi 2,000 wa Mtaa wa Kimondorosi, Kata ya Olasiti jijini Arusha, wamelalamikia kukosa huduma ya maji safi na salama kwa zaidi ya miezi mitatu mfululizo, hali inayowalazimu kutegemea maji ya mito na visima vya asili ambavyo si salama kiafya.

Wakizungumzia adha hiyo wananchi hao walisema hali hiyo imesababisha adha kubwa kwa familia na kusababisha migogoro ya kifamilia, ikiwemo wake na waume kulazimika kuamka usiku wa manane kutafuta maji.


“Sisi wananchi wa chini ndiyo tunateseka. Viongozi wetu wao hawana shida ya maji, ndio maana hawahangaiki nasi. Kwa miezi mitatu tumekuwa tukichota maji mtoni, jambo linalohatarisha afya zetu,” alisema Witness Ibrahimu, mkazi wa Kimondorosi.



Naye Bi. Betty Mtemi, mkazi wa eneo hilo, alisema tatizo la maji limekuwa sugu na kwamba mara chache maji yanapotoka ni usiku pekee, huku wakiendelea kubambikiziwa ankara za malipo ambazo hawajui zimetokana na huduma ipi.


“Ndiyo maana ndoa zetu zipo hatarini, maana kila usiku tunalazimika kutoka kwenda kutafuta maji. Maji hatupati, lakini ankara za kulipia maji tunaletewa kila mwezi. Hii ni dhuluma,” alisema kwa masikitiko.


Kwa upande wake, Felista Fabian, mkazi mwingine wa Kimondorosi, alisema hali hiyo imekuwa kikwazo kwa shughuli za kiuchumi za wakazi hao kwa kuwa muda mwingi wanapoteza kutafuta maji badala ya kujishughulisha na kazi za maendeleo.


“Wameniletea bili ya maji wakati miezi mitatu sijapata hata tone. Tunaomba Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, afike mtaani kwetu ashughulikie suala hili kwa sababu tumeshachoka. Hatuwezi kuendelea kulipa bili hewa bila huduma ya maji,” alisema.


Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimondorosi, Amani Ole Saluni, alithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa ameshawasiliana na viongozi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Auwsa), ambapo aliahidiwa kuwa huduma hiyo ingerejea ndani ya wiki mbili.


“Nilipata mawasiliano na Auwsa, wakaniambia kuwa baada ya wiki mbili maji yangerejea. Lakini hadi sasa ni zaidi ya miezi mitatu wananchi hawajapata huduma hiyo, hali ambayo inawaumiza sana,” alisema Ole Saluni.


Akizungumzia sakata hilo, Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameielekeza Auwsa kuhakikisha inatatua changamoto hiyo kwa haraka ili wananchi wa Kimondorosi na maeneo jirani wapate huduma ya maji bila usumbufu.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Auwsa, Mhandisi Justine Lujomba, alisema tayari wapo kwenye hatua ya mwisho ya kutatua changamoto hiyo kupitia mradi wa ujenzi wa tanki kubwa la maji lililofikia asilimia 98 ya ukamilishaji.


“Tanki hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 50,000 na litakapowekwa kwenye matumizi, huduma ya maji itapatikana kwa saa 24. Changamoto kubwa imekuwa ni maeneo yaliyo kwenye mwinuko kama Olasiti, hasa kipindi hiki cha kiangazi, lakini suluhisho liko karibu,” alisema Mhandisi Lujomba.


Jitihada za kufanikisha huduma hiyo zinatarajiwa kupunguza kero ya maji kwa wananchi wa Olasiti na maeneo ya jirani mara baada ya mradi huo kukamilika.



Ends...


Post a Comment

0 Comments