Na Joseph Ngilisho– ARUSHA
Mji wa Arusha umeendelea kuthibitisha nafasi yake kama kitovu cha mikutano na utalii barani Afrika baada ya kufanyika kwa Kongamano la Kimataifa la Utalii 2025, likiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yanayotarajiwa Septemba 27 mwaka huu.
Akifungua rasmi kongamano hilo leo jumatano Septemba 24,2025 Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, alisema lengo kuu ni kujenga jukwaa la kujadiliana, kushirikiana uzoefu na kuibua mawazo mapya yatakayosaidia kuboresha mustakabali wa utalii nchini.
> “Kupitia kongamano hili tunapata mrejesho wa mategemeo ya sekta ya utalii. Hii inatupa nafasi ya kujipanga vizuri zaidi katika kutoa wataalamu wanaoendana na mahitaji ya sasa na muelekeo wa sekta hii,” alisisitiza Prof. Sedoyeka.
Aliongeza kuwa IAA imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya utalii kupitia utoaji wa taaluma ya Utalii na Ukarimu, ikiwanda wa kuzalisha wahitimu wenye ubobezi na umahiri wa kuendeleza sekta hiyo kwa vitendo.
Wadau wa utalii waliohudhuria pia walipongeza hatua ya IAA kuandaa kongamano hilo, wakieleza kuwa limefungua ukurasa mpya wa majadiliano ya kitaaluma na kitaifa.
Kwa ujumla, kongamano la mwaka huu limeonesha dhamira ya Arusha siyo tu kama mji wa kitalii, bali pia kama kitovu cha fikra na dira mpya za maendeleo ya utalii. Wadau waliokutana wamesisitiza mshikamano, ubunifu na matumizi ya teknolojia kama nyenzo muhimu za kuimarisha sekta hii yenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.
-Ends..
0 Comments