UZINDUZI WA JOGGING YA WAZEE ARUSHA,WAZEE KUONESHANA KAZI , MPIRA WA SIMBA NA YANGA KUPIGWA NI BURUDANI YA KIHISTORIA!

 Wazee wa Arusha Wazindua Jogging na Bonanza la Michezo

Na Joseph Ngilisho– ARUSHA 

MASHARIKI wa michezo jijini Arusha wanatarajia kushuhudia burudani ya aina yake Jumamosi hii katika Bonanza la Wazee litakalofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Olasiti.

Bonanza hilo linaloandaliwa na jiji la Arusha,litaanza kwa mbio za jogging za wazee umbali wa kilometa 5, kisha kufuatiwa na mechi ya soka ya kusisimua kati ya mashabiki wa klabu kongwe za Simba na Yanga – zote zikishirikisha wapenzi wa michezo wenye umri wa dhahabu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Utamaduni wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, alisema lengo la mbio hizo ni kuimarisha afya za wazee pamoja na kuendeleza mshikamano katika jamii.


Alisema Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Joseph Mkude anatazamiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa klabu ya joging ya wazee itakayofanyika jumamosi hii kata ya Olasiti.


Lengo la kuanzishwa kwa klabu hiyo ni kutoa nafasi kwa wazee kushiriki shughuli za michezo kwa ajili ya kuimarisha afya.

“Tunawakaribisha wazee wote kushiriki. Hii siyo tu burudani, bali pia ni sehemu ya kujali afya zetu na kuimarisha undugu wa kijamii,” alisema Maneno.

Jogging itaanza saa 12:00 asubuhi, ikifungua pazia la burudani kwa wakazi wa Arusha. Baada ya hapo, macho yatageukia kwenye uwanja wa mpira, ambapo wazee mashabiki wa Simba na Yanga watashuka dimbani kuonyesha “uchawi” wao wa kandanda.

Mechi hiyo inatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki kutokana na ushindani wa jadi baina ya timu hizo mbili kubwa nchini.

Baadhi ya wazee waliopata nafasi ya kujiandaa na bonanza hilo wameonyesha shauku kubwa.

Mzee Isaya Kaaya (67) mkazi wa Olasiti alisema,"Hii jogging imenipa moyo mkubwa. Ukimbie na marafiki zako hata ukiwa na miaka mingi, unajisikia kijana tena. Natarajia kuona Simba yangu ikishinda, lakini zaidi ni furaha ya kushiriki.”

Wadau wa michezo jijini Arusha wamesema bonanza hilo litakuwa historia mpya ya michezo kwa wazee na litatoa hamasa kubwa kwa vizazi vyote kushiriki katika michezo kwa ajili ya afya bora na mshikamano.

Kwa ujumla, Jumamosi hii itakuwa siku ya kicheko, burudani na mshangao, huku viwanja vya Olasiti vikitarajiwa kujaa shamrashamra za michezo na upendo wa kijamii.

Ends..

Post a Comment

0 Comments