VERO AMKATA MUME UUME NA KUUTUPA NJE, AJISALIMISHA POLISI

VERO AMKATA MUME UUME NA KUUTUPA NJE, AJISALIMISHA POLISI

Na Joseph Ngilisho-– Manyara


WANANCHI wa Kijiji cha Kidangu, Kitongoji cha Maweni, Kata ya Endagaw wilayani Hanang’, mkoani Manyara wameshtushwa na tukio la kikatili ambapo mwanamke mmoja alimuumiza vibaya mume wake kwa kumkata sehemu zake za siri na kuzirusha nje ya nyumba usiku wa kuamkia Septemba 19, 2025.


Mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Veronica Muhale (40) anadaiwa kumvamia mume wake Josephati Kasi maarufu kama Khalidi Kasi (45) wakati akiwa amelala, akamfunga kwa kamba na shuka kitandani kisha kumkata kwa kisu sehemu zake za siri.


Chanzo cha tukio


Kwa mujibu wa taarifa, chanzo cha tukio hilo linadaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi uliodumu kwa muda mrefu. Mashuhuda walisema Veronica alikuwa akimtuhumu mume wake kwa usaliti, na awali alishawahi kujaribu kumdhuru kwa sumu ya panya bila mafanikio.


Aidha, inadaiwa kuwa kisu alichotumia alikihifadhi muda mrefu akipanga shambulio hilo.


Baada ya tukio


Mara baada ya kutekeleza unyama huo, Veronica alijisalimisha mwenyewe katika Kituo cha Polisi cha Katesh, akibainisha kuwa yeye ndiye aliyefanya kitendo hicho na kuwaomba ndugu na jamaa wasimsake.


Mumewe, Josephati, alikimbizwa kwa dharura katika Hospitali ya Mkoa wa Manyara kwa ajili ya matibabu, ambapo hali yake inaendelea kufuatiliwa na madaktari.


Tuhuma za kushirikiana


Wapo wanaodhani kuwa huenda Veronica hakutekeleza shambulio hilo peke yake, kutokana na hali yake ya kiafya, ingawa Polisi bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wa madai hayo.


Kauli za wananchi


Mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la Mama Daudi alisema tukio hilo limewaacha katika taharuki kubwa.

"Tuliamka asubuhi tukashangaa kusikia mwanamke kamkata mume wake uume… hii ni mara ya kwanza kuona unyama wa aina hii kijijini kwetu," alisema kwa masikitiko.


Jeshi la Polisi mkoani Manyara limesema uchunguzi wa awali unaendelea na litatoa taarifa kamili mara utakapokamilika.

Ends..


Post a Comment

0 Comments