KISERIANI YAANZA KWA SHANGWE, YAIPIGA MLANGARINI 1–0 KWENYE UFUNGUZI WA “MLANGARINI VIJANA SUPA LIGI”
Na Joseph Ngilisho–ARUMERU
MASHINDANO ya mpira wa miguu yajulikanayo kwa jina la Mlangarini Vijana Supa Ligi yamezinduliwa rasmi leo katika Kata ya Mlangarini, mkoani Arusha, kwa mchezo wa ufunguzi uliowakutanisha wenyeji Mlangarini FC dhidi ya Kiseriani FC, ambapo Kiseriani iliibuka na ushindi wa bao 1–0.
Mashindano haya yameandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya udhamini wa mgombea udiwani wa Kata ya Mlangarini, Emmanuel Mrema, yakilenga kuinua vipaji vya vijana, kuimarisha afya na mshikamano wa kijamii.
![]() |
Emmanueli Mrema ,Mgombea Udiwani Mlangarini |
Akizungumza baada ya mchezo, Mrema alisema mashindano hayo pia ni maandalizi ya vijana kuelekea kushiriki michuano mikubwa ya mpira wa miguu jijini Arusha mara baada ya kukamilika kwa uwanja wa kisasa unaoendelea kujengwa.
>
“Michezo ni sehemu ya ilani ya CCM. Kupitia ligi hii tumewaita pia wataalamu wa michezo kutambua na kukuza vipaji vya vijana wetu, kwani tunataka kuona wanasoka wanaochipukia kutoka Mlangarini wakipenya hadi kitaifa na kimataifa,” alisema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana UVCCM Kata ya Mlangarini, Hosea Malick Mollel, alisema mashindano hayo ni kielelezo cha mshikamano na dira ya kuendeleza vijana.
> “Hii ligi ni matokeo ya mshirikiano wa vijana wetu. Tunampongeza Mrema kwa kusimama bega kwa bega nasi. Tutaendelea kuhakikisha mashindano haya yanakuwa endelevu ili vijana wa Mlangarini waepukane na changamoto za mitaani na waone michezo kama sehemu ya maisha yao,” alisema.
Mchezaji wa Kiseriani, Emmanuel Godfrey, alisema ushindi wa leo umewapa morali ya kupambana zaidi kwenye michezo inayofuata.
>
“Tumefurahi kuanza na ushindi. Tunaamini ligi hii itatufungua milango ya kushiriki mashindano makubwa na hata kufikiwa na makocha wakubwa. Tunataka kuonyesha vipaji tulivyonavyo,” alisema.
Kwa upande wake, Augustino Mollel wa Mlangarini FC licha ya kichapo, alisema wao hawajakata tamaa.
>
“Tumepoteza mchezo wa kwanza, lakini bado tuna nafasi. Mashindano haya yametupa jukwaa la kuonyesha uwezo wetu na tunapambana kuhakikisha tunarejea kwa nguvu,” alisema.
Wananchi waliohudhuria mchezo wa leo walimpongeza mgombea udiwani Emmanuel Mrema kwa ubunifu na mchango wake katika kuleta burudani na mshikamano wa kijamii kupitia michezo.
John Mollel, mkazi wa Mlangarini, alisema
>“Tunamshukuru sana Mrema kwa kutuletea ligi hii. Vijana sasa wana nafasi ya kujionyesha badala ya kukaa mitaani. Tunataka mashindano kama haya yawe ya kudumu,” alisema.
Naye Rehema Laizer, mama wa vijana wawili wanaoshiriki ligi hiyo, aliongeza:
>
“Michezo ni burudani lakini pia kinga dhidi ya uhalifu na ulevi. Vijana wakiwa na shughuli kama hizi hawawezi kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa. Tunamuomba Mrema na wadau wengine waendelee kutuunga mkono,” alisema.
Ligi hiyo itaendelea kwa mfumo wa makundi, na michezo inatarajiwa kuchezwa kila wiki, ikiwakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Mlangarini. Wananchi wameombwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji vipya na kuunga mkono jitihada za kuinua michezo vijijini.
Ends..
0 Comments