Askari Magereza Njombe Ajitoa Uhai Baada ya Kukanwa na Mauaji ya Mwenzake
By Arushadigital-NJOMBE
Njombe imegubikwa na simanzi baada ya Askari wa Jeshi la Magereza, Erasto Mlelwa (26) mwenye namba C.916 WDR,pichani kulia kufariki dunia kwa kujirusha kutoka kwenye gari la Polisi wakati likiwa kwenye mwendo kasi. Tukio hilo limetokea muda mfupi baada ya mwili wa askari mwenzake aliyedaiwa kuuawa naye kupatikana.
Kauli ya Kamanda wa Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa Mlelwa alichukua uamuzi huo wakati Polisi walipokuwa wakimpeleka Hospitali ya Lilondo, wilayani Madaba mkoani Ruvuma, kwa ajili ya uchunguzi wa mwili wa askari mwenzie.
“Mtuhumiwa baada ya kuona mambo yako wazi aliamua kujitoa uhai wake kwa kuruka kutoka kwenye gari na kuangukia kichwa. Alipofikishwa hospitalini tayari alikuwa amepoteza maisha,” alisema RPC Banga.
Mwili wa Mwamakula Wapatikana Shambani
RPC Banga alifafanua kuwa uchunguzi wa awali ulianza baada ya kutoweka kwa Askari Magereza Dickraka Mwamakula (24) mwenye namba C.681 WDR, ambaye alipotea tangu Septemba 7, 2025. Taarifa zilionyesha kuwa kwa mara ya mwisho alionekana akiwa na Mlelwa katika eneo la Lilondo walipokwenda kuangalia mashamba.
Baada ya jitihada za upelelezi, mwili wa Mwamakula ulipatikana shambani akiwa amefukiwa, huku ukiwa na jeraha kubwa kisogoni na kuonesha dalili za kuchomwa moto.
Chanzo
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, inadaiwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kikazi. Marehemu Mlelwa anadaiwa kumuonea Mwamakula husuda kutokana na kupendwa na viongozi wake kwa utendaji mzuri wa kazi.
Ends..
0 Comments