Kanali Mstaafu JWTZ Aomba Rais Samia Ampe Jukumu la Kumfuta Machozi
Na Joseph Ngilisho, Arumeru
KANALI mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Joel Meidimi, ambaye aliwahi kuwa mtia nia wa ubunge Jimbo la Arumeru Magharibi, ameibuka na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan ampe jukumu la utumishi serikalini au ndani ya chama ili “kumfuta machozi” baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea.
Akihutubia wananchi katika uzinduzi wa kampeni za CCM Jimbo la Arumeru Magharibi, Kanali Meidimi alisema alikuwa na imani kubwa kwamba angepewa nafasi ya kugombea ubunge, lakini heshima ya chama na uamuzi wa vikao aliukubali kwa moyo mkunjufu.
> “Mimi mnayeniona hapa nilikuwa Kanali wa JWTZ. Nimetumika katika ngazi mbalimbali kwa uaminifu mkubwa hadi kustaafu mwaka 2021 nikiwa na nguvu kubwa. Nilipoona bado nina nguvu, niliwahi kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, ingawa sikupata. Nilipojaribu tena ubunge, pia sikupata, lakini bado nipo tayari kulitumikia taifa,” alisema.
Amesema kwa umri wake wa miaka 57 bado ana nguvu na uwezo wa kufanya kazi yoyote atakayoaminiwa na chama au serikali, huku akimsihi Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, kumtazama kwa fursa nyingine za uongozi.
> “Naomba Mheshimiwa Wasira, kwa heshima na taadhima, ikikupendeza katika chaguzi zako, unione kama naweza kutumika katika nafasi yoyote serikalini au ndani ya chama,” alisema Kanali Meidimi.
Kauli hiyo iliibua shangwe miongoni mwa wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano huo, ambapo mshikamano wa pamoja na kumuunga mkono mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dkt. Johannes Lukumay, ulitawala.
-ends..
0 Comments