Benki ya Baroda Yagusa Moyo kwa Watoto Yatima Arusha
Na Joseph Ngilisho, Arusha
BENKI ya Baroda tawi la Arusha imeendelea kutekeleza wajibu wake wa kijamii kwa kutoa msaada wa vyakula na magodoro kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha E.Venerate Orphanage, hatua iliyolenga kuwafariji watoto na kusaidia jitihada za serikali katika kuinua makundi yenye uhitaji.
Meneja wa tawi la benki hiyo mkoani Arusha, Gabinus Polepole, alisema msaada huo umetokana na kuguswa na hali ngumu ya maisha wanayopitia watoto hao. Alisema benki imekuwa ikitenga sehemu ya faida yake kila mwaka kwa ajili ya kusaidia jamii, ikiwa ni sehemu ya nguzo zake za uwajibikaji wa kijamii.
> “Tumeguswa na maisha ya watoto hawa, hivyo tumeamua kutoa sehemu ya faida yetu kuunga mkono serikali katika jitihada za kuyainua makundi yasiyojiweza. Ni jukumu letu kama taasisi kuhakikisha jamii inafaidika na uwepo wetu,” alisema Polepole.
Kwa upande wake, msimamizi wa kituo hicho, Safi Maliaki, aliishukuru Benki ya Baroda kwa msaada huo, akibainisha kuwa kituo kina jumla ya watoto 68 wanaosoma shule za msingi na sekondari.
Hata hivyo, Maliaki alieleza changamoto kubwa inayokikabili kituo hicho ni uhaba wa chakula, hali inayowalazimu watoto wakati mwingine kushindia uji pekee au kulala njaa.
> “Wakati mwingine tunakula uji tu asubuhi na mchana tunalala njaa. Kuna siku tunakosa kabisa chakula na kulala tumbo likiwa tupu. Tunakosa nguo na sare za shule, na usiku baridi hutuumiza kwa sababu hatuna mablanketi ya kutosha. Lakini msaada huu umetufariji sana na umetufanya tuone bado wapo watu wanaotufikiria,” alisema mmoja wa watoto kwa niaba ya wenzake.
Watoto hao walipokea msaada huo kwa furaha kubwa, wakionekana kutabasamu huku wakiimba nyimbo za shukrani kwa wageni waliowafikishia msaada.
> “Tunawashukuru sana Benki ya Baroda, kwa kweli mmetugusa mioyo yetu. Leo tumefurahi, tumepiga nyimbo na kucheza kwa sababu msaada huu umetufanya tuamini maisha yetu yana thamani,” aliongeza mtoto mwingine.
Maliaki alihitimisha kwa kusema msaada huo ni kama muujiza, kwani siku ya kupokea walikuwa wamechemsha maharage pekee bila kujua wangeongeza nini zaidi kwa chakula cha siku hiyo.
Ends...
0 Comments