CCM Yazindua Kampeni Kata ya Levolosi kwa Kishindo
Na Joseph Ngilisho – Arusha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Levolosi jijini Arusha kimezindua rasmi kampeni za uchaguzi, huku mgombea wa udiwani, Abbas Haji, akiweka bayana kipaumbele chake katika kutatua changamoto za masoko na msongamano wa magari unaowakabili wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza leo Septemba 5,2025 mara baada ya kutambulishwa na kukabidhiwa Ilani ya CCM na Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Arusha, Ramsey Saipulani, Haji aliahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani kwa vitendo ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Levolosi.
> “Nitajitahidi kuhakikisha tunapata utaratibu bora wa masoko. Hii itawapa wafanyabiashara wengi zaidi nafasi ya kufanya biashara kwa heshima na kuondokana na hali ya kufanya biashara barabarani,” alisema Haji.
Mgombea huyo pia aliahidi kushirikiana kwa karibu na Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha kero za wananchi, ikiwemo tatizo la msongamano mkubwa wa magari hasa katika eneo la Soko la Kilombero, zinapatiwa suluhu la kudumu.
Haji, ambaye kabla ya uteuzi wake alikuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Levolosi, alisema uelewa wake wa changamoto za wananchi wa eneo hilo utamsaidia kusukuma mbele mipango ya maendeleo na kupunguza kero zinazokwamisha maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Ramsey Saipulani, aliwataka wagombea wote wa udiwani kuacha tabia ya kulalamikia posho na badala yake wajikite katika kuwatumikia wananchi waliowaamini na kuwachagua.
> “Wananchi wanataka matokeo na suluhu ya matatizo yao. CCM haitarajii kuona madiwani wake wanabweteka baada ya kuchaguliwa, bali kila mmoja lazima asimamie Ilani na kuhakikisha wananchi wananufaika na uongozi wao,” alisema Saipulani
Kampeni hizo zilizozinduliwa katika eneo la soko la Kilombero ,zimeashiria mwanzo wa mbio kali za kisiasa katika Kata ya Levolosi, huku wananchi wakiahidi kushirikiana kwa karibu na mgombea huyo endapo ataibuka kidedea kwenye uchaguzi huo.
Mwisho
0 Comments