MASKINI LISU YAPINGAMIZI YAKE YATUPWA TENA,KESI KUENDELEA

Na Arushadigtal -Dar es Salaam

Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, imetupilia mbali hoja zote za mapingamizi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kuhusu ubatili wa hati ya mashtaka inayomkabili katika kesi ya uhaini.

Lissu alikuwa amedai kuwa hati hiyo ni batili kwa madai kwamba haioneshi maelezo ya kosa, wala nia ya kutenda kosa la uhaini — vipengele ambavyo ni muhimu kisheria katika hati ya mashtaka.

Hata hivyo, katika uamuzi uliosomwa leo, Septemba 22, 2025, na Kiongozi wa Jopo la Majaji, Jaji Dunstan Ndunguru, Mahakama ilibainisha kuwa hati ya mashtaka iko sahihi kwa mujibu wa sheria. “Hati hii inatoa maelezo ya kosa kama sheria inavyotaka, na suala la nia ya kutenda kosa ni jambo la ushahidi litakalojadiliwa wakati wa kusikilizwa kwa kesi yenyewe,” alisema Jaji Ndunguru.

Kuhusu hoja ya Lissu kuwa maelezo ya mashahidi ni batili kutokana na kudaiwa kukiuka amri ya Mahakama Kuu ya kuwalinda mashahidi wa Jamhuri ambao ni raia, pamoja na madai kuwa maelezo ya askari Polisi yalichukuliwa kinyume cha sheria, Mahakama ilieleza kuwa hoja hizo zinahusu mwenendo wa kabidhi (committal proceedings), jambo ambalo tayari liliwahi kutolewa uamuzi.

Mahakama ikahitimisha kwa kueleza kuwa pingamizi la Lissu halina msingi wowote kisheria na hivyo limetupwa rasmi, na kusisitiza kuwa kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa kama ilivyopangwa.

Ends..

Post a Comment

0 Comments