Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amefichua kuwa amewahi kulishwa sumu na kulazwa hospitalini, jambo lililosababisha kutoonekana kwake hadharani kwa kipindi cha muda mrefu.
Akizungumza jana Jumapili, Septemba 21, 2025, wakati wa ibada katika Kanisa la Mbingu Duniani lililopo Njiro – Arusha, Makonda alisema tukio hilo si mara yake ya kwanza, akidai kuwa amenusurika kifo mara kadhaa kutokana na mashambulizi ya aina hiyo.
"Kuna kipindi nilipotea hapa mjini nikiwa mkuu wa mkoa wa Arusha, na nikaanza kutafutwa, na wengine mlinitafuta kwa nguvu kubwa, ukweli nilikuwa naumwa, nililishwa sumu, yasingekuwa maombi ya Watanzania na Mungu kumuinua Rais Dkt. Samia Suluhu Haasan kusimamia matibabu yangu, nilitakiwa nife mwaka jana...
...ninapokuja mbele yenu kwa unyenyekevu mkubwa nikiwambia nahitaji maombi, mengine sina nafasi yakuyaeleza, lakini wako watu walitamani kuondoa uhai wangu katika nyakati tofauti tofauti” Mgombea Ubunge jimbo la Arusha Mjini (CCM), ndugu Paul Makonda akizungumza kwenye ukumbi wa Huduma ya Mbingu Duniani, Septemba 21, 2025.
Alimshukuru pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia matibabu yake nje ya nchi, akisema bila msaada na uamuzi wa Rais, leo hii angekuwa marehemu.
Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo, Askofu Emmanuel Michael, alimpongeza Makonda kwa ujasiri wa kushuhudia hadharani yaliyompata, akisema: “Hii ni ishara ya imani thabiti. Tumeshuhudia jinsi Mungu alivyo mwaminifu kwa kumuinua tena. Tunaamini ataendelea kumlinda katika majukumu yake mapya.”
Baadhi ya waumini nao walionyesha mshangao na faraja baada ya kusikia simulizi hiyo,Sarah John, mkazi wa Njiro, alisema: “Tuliwahi kujiuliza sana Makonda yupo wapi. Leo tumefarijika kwa kuwa tumemsikia mwenyewe akieleza alichopitia na jinsi Mungu na Rais Samia walivyomsaidia.”
Kwa upande wake, kijana Michael Daudi, alisema tukio hilo limewajenga vijana wengi kuona umuhimu wa imani na mshikamano wa kitaifa. “Makonda ni kioo chetu, tutaendelea kumuombea na kumuunga mkono katika safari yake ya kisiasa,” alisema.
Makonda alimaliza hotuba yake kwa kusisitiza kuwa tukio alilopitia limempa nguvu mpya na imani ya kusimama imara, huku akiwataka wananchi wa Arusha Mjini kuendelea kumuombea na kushirikiana naye kwa ustawi wa taifa.
Ends
0 Comments