MAGARI YA KAMPENI YA MAKONDA YAZUA GUMZO JIJINI ARUSHA NI MFANANO WA KIJESHI WANANCHI WASHANGAA,CCM YATOA UFAFANUZI!!

Magari ya Kampeni ya Paul Makonda Yazua Gumzo Jijini Arusha

Na Joseph Ngilisho– Arusha


Magari ya kampeni ya mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, yamezua gumzo mitaani na barabarani jijini Arusha, baada ya kuonekana yakipita yakiwa na mwonekano wa kipekee unaofanana na ule wa magari ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Wananchi walioshuhudia magari hayo walisema mwonekano wake wa rangi za mabaka mabaka uliofanana na magari ya kijeshi uliwafanya wengi kubaki wakiangalia kwa mshangao, huku baadhi wakihisi huenda ni magari ya jeshi yaliyotumika katika kampeni.




Akizungumzia hali hiyo, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Saipulani Remsey, alikanusha madai ya magari hayo kuwa ya kijeshi, akieleza kuwa ni ubunifu wa kampeni unaolenga kutoa mwonekano tofauti na wa kuvutia.

> “Huo ni ubunifu wa kawaida wa mgombea. Hakuna ukweli kwamba magari hayo ni ya kijeshi. Yamenakshiwa kwa rangi zetu za chama, bluu na njano, ila yamewekwa kwa namna ya kipekee ili kuonekana tofauti. Ni mbinu ya kubadili mwonekano wa kampeni,” alisema Remsey.


Aidha, Remsey aliongeza kuwa chama hakina mamlaka ya kumpangia mgombea aina ya usafiri anaotumia katika kampeni zake.

> “Hatuwapangii wagombea wetu watumie usafiri gani. Kinachofanyika ni ubunifu wa mtu mmoja mmoja, na tunaheshimu namna kila mgombea anavyotaka kuwasilisha taswira yake mbele ya wananchi,” alisisitiza.


Wakati baadhi ya wananchi waliona magari hayo kama mvuto mpya wa kisiasa, wengine walieleza hofu yao juu ya rangi zinazofanana na zile za JWTZ.

Neema John, mkazi wa Sekei, alisema,"Nilipoyaona mara ya kwanza nilidhani ni magari ya jeshi. Lakini baada ya kusikia ni ya kampeni, nikajua ni ubunifu tu. Kwa kweli yamekaa vizuri na yanavuta macho.”


Kwa upande wake, Mussa Ngariba, mkazi wa Unga Limited, alisema,"Kampeni siyo lazima zifanane kila wakati. Hata hivyo, ingekuwa vizuri mgombea akatumia rangi zinazotambulika moja kwa moja na chama ili kuepusha mkanganyiko.”


Mchambuzi wa masuala ya kisiasa jijini Arusha, Dkt. Hamisi Lema, alisema ubunifu wa aina hii katika kampeni ni mkakati wa kisaikolojia unaolenga kuvuta hisia na kuleta taswira ya nguvu.

> “Wagombea wengi hutumia mbinu za kustaajabisha ili kutengeneza mjadala wa umma. Mwonekano wa kijeshi unaweza kumsaidia mgombea kuonekana mwenye uthabiti na ushawishi, lakini pia unaweza kuibua tafsiri tofauti miongoni mwa wananchi, hasa wale wanaohusisha moja kwa moja na jeshi,” alisema Dkt. Lema.


Aidha, aliongeza kuwa katika siasa za kisasa, picha na mwonekano mara nyingi huchukua nafasi kubwa kuliko ujumbe wa maneno pekee.


> “Kampeni si tu hotuba na sera, bali pia ni taswira. Magari haya tayari yamempa Makonda umaarufu wa haraka mitaani, jambo linaloweza kuwa na faida katika kumtambulisha zaidi kwa wapiga kura,” aliongeza.


Huku mijadala ikiendelea mitaani na kwenye mitandao ya kijamii, wachambuzi wanasema ubunifu wa aina hiyo unaweza kuwa na faida ya kuongeza ushawishi wa kisiasa, lakini pia unahitaji tahadhari ili usigeuke kikwazo.

Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwenye kampeni za Makonda jijini Arusha, zikisubiriwa kuona ni ubunifu gani mwingine mpya ataibua katika mbio za kuelekea uchaguzi.








-ends....

Post a Comment

0 Comments