CCM Yatangaza Ujio wa Mgombea Mwenza wa Urais, Dkt. Nchimbi, Mkoani Arusha
Na Joseph Ngilisho-– Arusha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi ziara ya mgombea mwenza wa urais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, mkoani Arusha, itakayofanyika Septemba 12, 2025, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo septemba 10,2025 ofisini kwake jijini Arusha, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM mkoa huo, Saipulani Remsey, alisema maandalizi yote yako tayari na chama kinatarajia mapokezi makubwa kutoka kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
> “Tunawakaribisha wananchi na wafuasi wa CCM kuujaza uwanja wa Soweto. Huu ni mkutano wa kihistoria ambapo Dkt. Nchimbi atamwombea kura Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda,” alisema Remsey.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Dkt. Nchimbi ataanzia ziara yake wilayani Longido saa mbili asubuhi, kisha ataelekea Arumeru saa tano asubuhi ambapo atafanya mkutano katika barabara ya Bypass. Ziara hiyo itahitimishwa kwa mkutano mkubwa jijini Arusha utakaofanyika katika Uwanja wa Soweto kuanzia majira ya saa saba mchana.
Remsey alisisitiza kuwa CCM imedhamiria kuhakikisha wananchi wanahudhuria kwa wingi bila vikwazo vya usafiri.
> “Sasa hivi tunatumia mabasi kuwabeba wafuasi wetu na siyo tena punda. Tunawahakikishia usafiri wa uhakika ili kila mmoja afike kwa wakati. Raha ya mwanasiasa ni kuona uwanja umefurika wananchi wenye hamasa,” aliongeza huku akisisitiza mshikamano wa chama hicho tawala.
Katika hatua nyingine Remsey alisema kuwa mkutano huo utapambwa na magari yenye rangi za mabakamabaka ya mgombea Ubunge wa jimbo la Arusha,Paul Makonda ,na kuwatoa hofu wananchi wanaohofia kwamba ni magari ya jeshi la wananchi JWTZ.
Baadhi ya wafuasi wa CCM jijini Arusha wameeleza matarajio yao kuhusu ujio wa Dkt. Nchimbi, wakisema ni fursa ya kuimarisha mshikamano ndani ya chama.
> “Tunatarajia kusikia mipango ya chama chetu kuendelea kuboresha maisha ya wananchi. Ujio wa Dkt. Nchimbi unatupa matumaini makubwa ya ushindi.”
Kwa upande wake, Jackson Mollel, kijana kutoka Ngaramtoni, alibainisha kuwa ziara hiyo imewapa nguvu mpya vijana kuendelea kushiriki kwenye kampeni.
> “CCM ni chama chetu na ujio huu unatuamsha zaidi. Vijana tupo tayari kushirikiana kuhakikisha ushindi wa Rais Samia na wagombea wetu unapatikana.”
Chama hicho kimeeleza kuwa ziara ya Dkt. Nchimbi inalenga kuimarisha kampeni za urais na ubunge katika Mkoa wa Arusha, sambamba na kuwaunganisha wanachama katika kushiriki kikamilifu mchakato wa uchaguzi ujao.
Ends..


0 Comments