KISILA ATIKISA KAMPENI SEKEI ,AAHIDI AFYA,ELIMU NA AJIRA KWA VIJANA!

 Kisila Azindua Kampeni Sekei, Aahidi Afya, Elimu na Ajira kwa Vijana

Na Joseph Ngilisho– Arusha

Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Sekei, Emmanuel Kisila, ameahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo, huku akitilia mkazo sekta za afya, elimu na mikopo ya kijamii ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Akizungumza leo September 14,2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Sanawari jijini Arusha wakati akizindua kampeni zake, Kisila alisema dhamira yake ni kuhakikisha wananchi wa Sekei wananufaika moja kwa moja na miradi inayotekelezwa na serikali ya CCM.

“Tutahakikisha huduma za afya zinaboreshwa, shule zinaimarishwa na mikopo ya akina mama na vijana inapatikana kwa wakati ili kuongeza kipato na ustawi wa familia zetu,” alisema Kisila huku akishangiliwa na umati wa wananchi.


Kisila alisisitiza pia kuwa miundombinu ya kata hiyo itapewa kipaumbele kwa kushirikiana na wananchi na halmashauri, ili kuboresha barabara na huduma nyingine muhimu zinazowawezesha wananchi kuendesha shughuli zao kwa urahisi.

Akizungumzia changamoto ya ajira kwa vijana, Kisila alieleza kuwa vijana wa Sekei ni rasilimali kubwa na lazima washirikishwe moja kwa moja kwenye maendeleo ya kata hiyo.

“Nitasimama bega kwa bega na vijana wa Sekei. Nitawashika mkono, kuwatafutia nafasi za ajira na pia kuwawezesha kupata mitaji ya kuanzisha biashara. Hii ni nguvu kazi ya taifa na hatuwezi kuiacha nyuma,” aliongeza.


Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo walionesha hamasa kubwa, wakimhakikishia Kisila ushirikiano wa karibu katika safari ya kuelekea ushindi wa CCM kata ya Sekei.

Ends..

Post a Comment

0 Comments