TUGHE YAWAKUTANISHA VIONGOZI NA WAAJIRI KWA MAFUNZO YA TEKNOLOJIA YA AKILI MNEMBA NA AFYA SEHEMU ZA KAZI


Na Joseph Ngilisho, Arusha


Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimeandaa mafunzo ya kipekee kwa viongozi wa matawi na waajiri zaidi ya 800 kutoka taasisi 300 za serikali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uwezo kuhusu matumizi ya Akili Mnemba (AI) na teknolojia za kidijitali katika kuboresha afya na usalama sehemu za kazi.


Mafunzo hayo, ambayo yalianza leo, Septemba 15, 2025, jijini Arusha, yataendelea kwa siku tano na yanatarajiwa kumalizika Septemba 19. Yamelenga kujenga uwezo katika masuala muhimu ya utawala, ikiwa ni pamoja na taratibu za uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma, usuluhishi wa migogoro ya kazi, maamuzi ya kiutumishi, na mchango wa mabaraza ya wafanyakazi katika kukuza tija kazini.



Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda, alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kugusa maeneo mbalimbali muhimu, ikiwemo mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia sehemu za kazi, afya ya akili, na umuhimu wa emotional intelligence kwa viongozi na wafanyakazi.


Akifungua mafunzo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Zuhura Yunus, aliipongeza TUGHE kwa ubunifu wa mafunzo hayo, akisema kuwa ni hatua muhimu katika kuboresha ufanisi wa serikali, wafanyakazi, na taasisi za umma.


“Ninaamini kuwa mafunzo haya yatasaidia kupunguza migogoro kazini na kuimarisha tija, kwani yanawaleta waajiri na wawakilishi wa wafanyakazi pamoja kuelewa sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma,” alisema Zuhura Yunus.


Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Joel Kaminyoge, alisisitiza kuwa mafunzo haya ni muhimu katika kuimarisha mahusiano kazini, kuongeza tija, na kupunguza migogoro. Aliongeza kuwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha utawala bora na kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao ipasavyo.



Kwa upande wake, mshiriki wa mafunzo hayo, Neema Swai, alieleza kuwa elimu hii ni muhimu kwa viongozi wa matawi kwani itawawezesha kupunguza migogoro sehemu za kazi. Alipongeza pia serikali kwa hatua ya kutoa likizo maalumu kwa mfanyakazi anapojifungua mtoto njiti, kuanzia wiki ya 40 ya ujauzito, akisema kuwa hatua hii itaboresha mazingira ya kazi kwa wanawake.


Mafunzo haya pia yanajumuisha safari ya kitalii ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa washiriki, ikiwa ni sehemu ya kujifunza kuhusu vivutio vya utalii nchini na kutoa fursa ya kupumzika na kujenga timu miongoni mwa washiriki.


TUGHE inatarajia kuwa mafunzo haya yataongeza ufanisi katika maeneo ya kazi, yakifungua njia ya maendeleo ya kiutawala na kuboresha mazingira ya kazi nchini Tanzania.

Ends

Post a Comment

0 Comments