ABRAHAM AWASHA MOTO KAMPENI KIMANDOLU,AAHIDI KATA YOTE KUFUNGWA TAA USIKU WANANACHI WAMBEBA JUU JUU,MEKU AMKABIDHI JEMBE LA KAZI

Mollel (Kobra) Azindua Kampeni Kimandolu, Aahidi Barabara, Elimu na Usalama

Na Joseph Ngilisho– Arusha

 

Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kimandolu jijini Arusha, Abrahamu Mollel maarufu kama Kobra, amezindua rasmi kampeni zake kwa kuahidi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kata hiyo.


Akihutubia mamia ya wakazi wa Kimandolu leo septemba 14,2025, Mollel alisema kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa miundombinu ya barabara, ambapo aliahidi kufanikisha kukamilika kwa kipande cha lami chenye urefu wa kilomita 1.5 kutoka ofisi ya CCM ya kata hiyo hadi Ngulelo ifikapo mwaka 2027.


Aidha, aliahidi kusukuma halmashauri kuhakikisha daraja la Riverside linajengwa ili liweze kupitika muda wote, jambo litakalorahisisha shughuli za wananchi hasa katika kipindi cha mvua.


Kwa upande wa elimu, Mollel alieleza kuwa ataendelea kushirikiana na serikali na wadau kuboresha mazingira ya kujifunzia. Aliahidi kushughulikia ujenzi wa hosteli katika shule ya sekondari Kimaseki, na kusisitiza kuwa tayari amefanikisha upatikanaji wa shilingi milioni 57 zilizojenga jengo la utawala katika shule ya msingi Suye, ambalo litazinduliwa iwapo atachaguliwa tena. Pia aliahidi kuendeleza ujenzi wa ukuta wa shule hiyo kwa ajili ya usalama wa wanafunzi.


Akigusia usalama wa wananchi, Mollel alisema atahakikisha nguvu kubwa inawekwa kudhibiti vitendo vya uhalifu ili kuondoa hofu ya vibaka katika kata hiyo.


 “Nitahakikisha barabara zote kubwa zinakuwa na taa zitakazowaka usiku kucha, ili wananchi waweze kuendelea na biashara zao hata nyakati za usiku bila hofu,” alisema.


Mollel aliahidi kushirikiana kwa karibu na wenyeviti wa mitaa ili kuhakikisha maendeleo yanayogusa wananchi yanapewa kipaumbele.


Katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM wilaya Ally Meku, alimnadi mgombea huyo na kumkabidhi ilani ya chama. Alitoa wito kwa wananchi wa Kimandulu kuendelea kuiunga mkono serikali ya CCM kutokana na utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo.


“Wananchi wenzangu, tumuunge mkono Mollel ili akamilishe miradi mikubwa aliyokwisha kuianzisha na kuendeleza mengine kwa manufaa ya wote,” alisema Meku.










Ends..


Post a Comment

0 Comments