Dkt. Lukumay Aeleza Vipaumbele vya Maendeleo Arumeru Magharibi
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
Mgombea ubunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Johannes Lukumay, leo Septemba 7, 2025 amezungumza na waandishi wa habari jijini Arusha na kuweka bayana vipaumbele vyake vya maendeleo endapo wananchi watamchagua kuongoza jimbo hilo.
Amesema dira yake ya uongozi inalenga sekta kuu mbili zenye mguso wa moja kwa moja katika maisha ya wananchi—afya na elimu, akibainisha kuwa ndizo nguzo za ustawi wa familia na maendeleo ya taifa.
“Wananchi wa Arumeru Magharibi wanapaswa kupata huduma bora za afya bila kikwazo cha miundombinu mibovu au uhaba wa wataalamu. Nimewaita leo kuwaeleza mipango ya maendeleo itakayobadilisha jimbo letu ambalo lina changamoto nyingi lakini pia lina fursa nyingi,” alisema Dkt. Lukumay.
Miundombinu ya Afya
Akibainisha ukubwa wa jimbo hilo lenye tarafa tatu, kata 27, vijiji 67, vitongoji 256 na kaya zaidi ya 72,000, Dkt. Lukumay aliorodhesha mikakati yake ya sekta ya afya, ikiwemo:
Kuboresha vituo vya afya vya Mbuyuni, Ulukokola na Uldonyosambu.
Kupanua zahanati za Likamba, Ulnjorous, Lemugur na Mungushi/Themi ya Simba.
Kuimarisha Hospitali ya Wilaya ya Uturumet kwa kujengewa uzio na kuongezewa madaktari bingwa.
Kununua magari matatu ya wagonjwa (ambulance) kwa vituo vya Songambele Bwawani, Mwandet na Uldonyosambu.
Kujenga vituo vipya vya afya katika kata za Sambasha, Kimunyak, Bangata na Musa.
“Huduma za afya si anasa bali ni haki ya kila Mtanzania. Nimeweka mikakati ya kuhakikisha kila kata inakuwa na huduma za uhakika, ili wananchi wasipoteze maisha kwa matatizo yanayozuilika,” alisisitiza.
Uboreshaji wa Elimu
Katika sekta ya elimu, mgombea huyo alieleza dhamira yake ya kuhakikisha kila kijana anapata fursa ya kusoma katika mazingira bora na salama. Miongoni mwa mikakati yake ni:
Ujenzi wa maabara mpya katika Shule ya Sekondari Ulkokola na kuboresha maabara ya Uturuto.
Ujenzi wa shule mpya za sekondari katika kata za Kiranyi, Larukwa na Ilboru.
Ujenzi wa mabweni katika shule za Ujoro Entees, Likamba na Losikito.
Kupanua na kupandisha hadhi shule za Ulmotonyi, Uldadai na Mateves.
Kuwahakikishia fidia stahiki wananchi wanaopisha maeneo ya ujenzi wa shule mpya.
“Elimu bora ndiyo tiketi ya vijana wetu kushindana katika dunia ya sasa. Tutawekeza kwenye miundombinu, walimu na usalama wa shule ili hakuna kijana wa Arumeru anayebaki nyuma,” alisema kwa msisitizo.
Wito kwa Wananchi
Akihitimisha mazungumzo yake, Dkt. Lukumay aliwaomba wananchi wa Arumeru Magharibi kushirikiana naye katika safari ya maendeleo, akisisitiza mshikamano wa kijamii kama msingi wa mafanikio.
“Ninaamini kwa mshikamano wa wananchi, Arumeru Magharibi itakuwa mfano wa maendeleo ya kisasa. Afya na elimu bora vitatufungulia milango ya ustawi na fursa za kiuchumi,” alisema kwa kujiamini.
Kauli zake zimeibua matarajio mapya miongoni mwa wananchi, huku akisisitiza kuwa dira yake inalenga kubadilisha maisha ya kila familia kupitia sekta zinazogusa moja kwa moja ustawi wa jamii.
Ends…
0 Comments